RAIS MAGUFULI AWATUMBUA WAKURUGENZI WAWILI WA HALMASHAURI

Rais John Magufuli amewasimamisha kazi wakurugenzi wawili wa halmashauri za Kigoma Ujiji, Boniface Nyambe na Daud Mlahagwa (Pangani).

Rais Magufuli ametoa uamuzi huo leo Jumanne Machi 27, 2018 wakati akipokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad iliyobaini madudu katika ukaguzi wa serikali za mitaa na mashirika ya umma.


“Kuanzia leo mkurugenzi wa Pangani na Kigoma Ujiji wasimamishwe kupisha uchunguzi, uchunguzi ufanyike kuanzia leo lazima tuchukue hatua,” amesema.


Akiwasilisha ripoti hiyo, Profesa Assad amesema serikali za mitaa 140 zilishindwa kukusanya mapato ya Sh116 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 22 ya mapato yake.


“Zaidi ya hayo pia tuliona mawakala kutowasilisha Sh3.5 bilioni ya makusanyo lakini hawakuwasilisha, ni usimamizi mbovu tu wa halmashauri kwani kama mawakala wamekusanya kwa nini usikusanye mapato yako,” amesema Profesa Assad.


Madudu mengine aliyobaini CAG ni kupotea kwa vitabu 379 vya mapato ya Serikali, ambavyo haikujulikana ni kiwango gani cha fedha kilichopotea kutokana na upotevu wa vitabu hivyo.


“Kitabu cha mapato kisipokuja kwetu hatuwezi kujua ni kiwango gani kimetumika katika vitabu hivyo, lakini tuliona katika halmashauri za Bihalamuro, Karagwe na Mpwapwa, kulikuwa na miradi mitatu ambayo thamani yake ilifikia Sh1.6 bilioni iliyocheleweshwa kukamilishwa,” amesema.


“Pia, kulikuwa na udhaifu katika usimamizi wa rasilimali watu na udhibiti wa mishahara, kwa mfano kuna madai ya watumishi ambayo yanafikia Sh10 bilioni katika mamlaka za serikali za mitaa 19, ambao hawakulipa hadi mwisho wa mwaka wa Juni 2017.”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527