Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HIFADHI YA TAIFA KISIWA CHA SAANANE YAADHIMISHA 'BIRTHDAY' MIAKA 10 YA SIMBA, MFALME WA PORI AFURAHIA KEKI MAALUM


Simba wa Keki maalum kwa ajili ya Simba wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane akijiandaa kula keki maalum
Keki maalum kwa ajili ya Simba wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane leo imeandika historia mpya katika sekta ya uhifadhi na utalii nchini Tanzania baada ya kuadhimisha miaka 10 ya simba wanaohifadhiwa katika kisiwa hicho, kupitia tukio la kipekee lililobeba kauli mbiu “Saanane King Turns Ten.”

Tukio hilo, ambalo ni la kwanza kufanyika katika hifadhi yoyote nchini, limefanyika Desemba 20,2025 katika Kisiwa cha Saanane kilichopo katikati ya Ziwa Victoria, jijini Mwanza, likilenga kuhamasisha utalii, kuongeza uelewa wa uhifadhi wa wanyamapori, na kuthibitisha nafasi ya hifadhi ndogo za mijini katika kukuza sekta ya utalii.

Katika maadhimisho hayo, wageni wamepata fursa ya kushuhudia tukio la nadra la kumlisha simba keki maalum iliyotengenezwa kwa malighafi salama kwa mnyama huyo, huku wakielimishwa kuhusu historia yake, mwenendo wa maisha, tabia zake, pamoja na nafasi yake katika kundi maarufu la “The Big Five.”

Akizungumza katika tukio hilo, Afisa Uhifadhi Daraja la Kwanza na Msimamizi wa Kitengo cha Utalii wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, Cesilia Nkwabi, amesema simba ni miongoni mwa wanyama wenye umuhimu mkubwa katika uhifadhi wa ikolojia na kivutio kikuu cha utalii.
Cesilia Nkwabi

“Simba ni mfalme wa nyika na mmoja wa wanyama maarufu barani Afrika na duniani. Kwetu kama hifadhi, ana mchango mkubwa sana katika uhifadhi, elimu ya mazingira na utalii. Kupitia maadhimisho haya ya miaka 10 ya simba wa Saanane, tunatoa wito kwa Watanzania na dunia kwa ujumla kuungana kulinda simba wote ili waendelee kuwepo kizazi hadi kizazi,” amesema Nkwabi.

Ameongeza kuwa simba ana nafasi muhimu katika kusawazisha mwingiliano wa ikolojia, kwa kudhibiti idadi ya wanyama wengine na kuhakikisha mifumo ya asili inaendelea kwa usawa.

Kwa upande wake, Mkuu wa  Kitengo cha Himasheria na Ulinzi Mkakati Pellagy Marandu akizungumza kwa niaba ya Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, amesema siku hii ni ya kihistoria kwa hifadhi hiyo na TANAPA kwa ujumla.
Pellagy Marandu

“Kwetu Saanane na TANAPA, leo ni siku muhimu sana. Simba wetu wamefikisha miaka 10, na kwa kutambua umuhimu wake tumeona tumpe heshima yake kwa kufanya sherehe hii. Tunamthamini mnyama Simba, Mfalme wa pori, ambaye ni kivutio kikubwa cha watalii,” amesema Marandu.

Maadhimisho hayo pia yamelenga kuongeza thamani ya utalii wa mijini (urban tourism) katika Mkoa wa Mwanza, kwa kuonyesha kuwa vivutio vya kipekee havipatikani tu katika hifadhi kubwa, bali pia katika hifadhi ndogo zilizo karibu na miji.

Katika tukio hilo, wageni hususan wanafunzi wamepata nafasi ya kushiriki maswali na majadiliano kuhusu uhifadhi wa wanyamapori, ambapo washindi wametunukiwa zawadi mbalimbali kama njia ya kuhamasisha elimu ya uhifadhi kwa kizazi kipya.
Baadhi ya watalii wa ndani walioshuhudia tukio hilo, akiwemo Japhet Boaz na Debora Japhet, wameipongeza Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane kwa kuandaa tukio hilo la kipekee linalochochea utalii wa ndani, huku wakiwahimiza Watanzania kuendelea kutembelea hifadhi za taifa ili kujifunza, kuburudika na kuelimika.

Nao wanafunzi wa Chuo cha Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi, akiwemo Naishon Ngarash Mollel, Safiel Elietiniswi Mnzava, Junior Mzamin Magwali na Ester Anjelo George, wamesema tukio hilo limewapa uelewa mpana kuhusu maisha ya simba, wakibainisha kuwa simba anayehifadhiwa ndani ya uzio anaweza kuishi hadi miaka 20, tofauti na simba wa porini.

Kwa upande wake, Mwongoza Wageni wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, Sanura Heri, ametumia fursa hiyo kuwaelimisha washiriki kuhusu tabia, makazi na umuhimu wa simba katika mfumo wa ikolojia.
Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane ni miongoni mwa maeneo adimu yanayosimamiwa na TANAPA, ikiwa na hadhi ya kipekee kama hifadhi ya kwanza Tanzania iliyopo katikati ya mji. Iko umbali wa dakika 10 tu kwa usafiri wa boti kutoka katikati ya Jiji la Mwanza, jambo linaloifanya kuwa kivutio rahisi na cha kipekee kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.

Kisiwa hicho kina ukubwa wa takribani kilomita za mraba 2.18, hivyo kuwa hifadhi ndogo kuliko zote nchini, lakini licha ya ukubwa wake mdogo, kina utajiri mkubwa wa viumbe hai na mandhari ya kuvutia, kikithibitisha kuwa uhifadhi na utalii vinaweza kustawi hata katika maeneo madogo yaliyo karibu na miji.

ANGALIA PICHA




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com