HATIMAYE NONDO AFIKISHWA MAHAKAMANI...ASAFIRISHWA USIKU KWENDA IRINGA


Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo amesafirishwa usiku wa kuamkia leo Machi 21, 2018 kupelekwa mkoani Iringa.


Taarifa zilizotolewa na wakili wake, Jebra Kambole leo Jumatano Machi 21, 2018 zinaeleza kuwa sasa Nondo yupo Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa.


Nondo anadaiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha Machi 6, 2018 na siku inayofuata akaonekana mjini Mafinga, wilayani Mufindi, Iringa ambako alishikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo na baadaye kurejeshwa Dar es Salaam.


Tangu akamatwe Nondo hajawahi kuzungumza na wakili wake wala mtu yeyote wa karibu yake jambo ambalo limekuwa likipingwa na watetezi wa haki za binadamu.


Jana, Jebra alisema kuwa wamefungua kesi kwa ajili ya kuiomba mahakama mambo matatu, kwanza kumpa dhamana Nondo, pili kutoa amri ya kuwapa mawakili haki ya kuonana na Nondo na kingine ni kuitaka mahakama itamke mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) ameshikiliwa kinyume cha sheria.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527