MWANAFUNZI UDSM APIGWA ONYO VITENDO VYA KUSHUSHA HADHI YA CHUO

Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, umempatia barua ya Onyo mwanafunzi Kumbusho Dawson Kagine kutokana na kujihusisha na vitendo tofauti na wajibu wake kama mwanafunzi.

Barua inayoaminika kuwa imetoka kwenye Uongozi wa Chuo Kikuu Mlimani imeeleza kuwa chuo kimepata taarifa ya kuwa Kumbusho ni miongoni mwa wanafunzi wanaojihusisha na vitendo kinyume na sheria za wanafunzi za chuoo hicho (UDSM Student By Laws 2011).

Imeelezwa kuwa vitendo ambavyo havikubaliki ni pamoja na kupanga na kuhamasisha maandamano kitu ambacho ni kinyume cha sheria ikiwa ni pamoja na kujihusisha na vitendo vinavyoshushia hadhi chuo hicho.

Aidha kwa mujibu wa barua hiyo Kumbusho ameonywa kuacha vitendo hivyo mara moja na endapo atakaidi atakuwa amejiongezea makosa mengine kama jinsi ilivyoainishwa kwenye sheria ndogondogo za wanafunzi.

"Unakumbushwa kuwa onyo hili ni la mwisho na endapo utaendelea kujihusisha na vitendo hivyo, moja kwa moja au kwa kuwashawishi, utasimamishwa masomo mara moja kulingana na kipengele cha 14(ix) wakati mashtaka yako dhidi yako yakiandaliwa na kushughulikiwa" Imeandikwa Sehemu ya barua hiyo.

Akithibitisha kutolewa kwa adhabu hiyo Afisa Mahusiano wa Chuo hicho Jackson Isdor amesema kuwa ni kweli Kumbusho amepatiwa onyo na uongozi wa chuo hicho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527