MAHAKAMA YAMSHIKA KOO MWANASHERIA MKUU KUHUSU MAANDAMANO TANZANIA

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imemuagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kuleta majibu kuhusu mashauri mawili ya kikatiba yaliyofunguliwa mahakamani hapo na wanaharakati dhidi ya ofisi yake, ifikapo Machi 21 mwaka huu.


Mashauri hayo ni, shauri namba 4/2018 linalopinga sheria ya jeshi la polisi na ya vyama vya siasa zinazodaiwa kuzuia mikutano ya vyama vya siasa, na shauri namba 6/2018 linalopinga sheria ya uchaguzi inayowapa mamlaka Wakurugenzi wa Halmashauri nchini (maded) kuwa wasimamizi wa uchaguzi.

Hayo yamebainishwa leo mahakamani hapo na Mwanasheria upande wa walalamikaji, Wakili Jebra Kambole baada ya kuairishwa kutajwa kwa tarehe za kesi hizo kufuatia majaji wanaosikiliza kutokuwepo mahakani kwa sababu ya kuwa na dharula.

Vile vile, Wakili Kambole amesema mahakama imetaja tarehe 5 Aprili, 2018 kuwa siku ya kutajwa tarehe za kesi hizo.

“Mahakama imetoa amri mbili, kwanza imetaja terehe 5 mwezi wa 4 haya mashauri yatakuja kutajwa tarehe, imetoa amri ya pili kwa mwanasheria mkuu wa serikali kwamba anapaswa kuleta majibu yake tarehe 21 mwezi wa 3, 2018 kwa hiyo hizo ni amri mbili zilizotolewa na mahakama siku ya leo. “

Amesema miongoni mwa walalamikaji katika shauri namba 4/2018 ni Baraka Mwago, wakati shauri namba 6/2018 mlalamikaji ni Bob Chacha Wangwe.

“Tulichokuja leo ni kuangalia namna gani mahakama itatoa amri ili watu mbalimbali waweze kutimiza wajibu wao, ni mashauri ya kikatiba yanapinga sheria mbalimbali ikiwemo sheria ya uchaguzi ambayo inafanya maded kuwa wasimamizi wa uchaguzi wakati inapaswa kuwa na tume huru ya uchaguzi, shauri namba nne inapinga sheria ya jeshi la polisi na sheria ya vyama vya siasa ambazo zinazuia mikutano ya vyama vya siasa na kuleta madharakwa wanachi. Tunapinga sheria hizo tunaona ni kandamizi zinakiuka katiba ikiwemo ibara ya 18 inayoruhusu uhuru wa kujieleza,” amesema na kuongeza.


“Inakiuka uhuru wa kufanya maamuzi juu ya maisha ya watanzania na maendeleo ya nchi yao, inakiuka haki ya kusikilizwa kwa watu ambao wakitaka kuandamana wanapata amri bila kusikilizwa, tunaangalia uhalali wa hizo sheria dhidi ya katiba ya nchi, kwa mujibu ibara ya 26 intoa jibu kwa mtu anayeona sheria yoyote iakiuka anawajibu wa kuleta shauri mahakamani, walalamikaji wametimiza wajibu wao kikatiba.”
Na Regina Mkonde

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527