KAMPENI YA KUPIMA UKIMWI WANAUME YAJA TANZANIA


Baada ya utafiti kubaini mwamko mdogo kwa wanaume kupima na
kutumia dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARVs), Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) sasa kuanzisha kampeni maalumu.

Akizungumza leo Jumapili Machi 25, 2018 na Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Kupambana na Dawa za Kulevya, mkurugenzi mkuu Tacaids, Dk Leonard Maboko amesema kampeni hiyo itakuwa miongoni mwa shughuli zitakazofanywa katika mkakati wa nne wa kupambana na Ukimwi nchini.

“Katika utafiti wa mwaka 2016/17, tuliangalia vitu vipya ambavyo ni maambukizi mapya na kiwango cha kufubaza VVU. Tuligundua ingawa wanawake wanaongoza katika maambukizi mapya, lakini ni wepesi kupima na kutumia dawa kikamilifu ndiyo maana kwenye kiwango cha kufubaza wanaongoza,”amesema.

Amesema katika utafiti huo uliozinduliwa Desemba mwaka jana, kiwango cha watu kufubaza VVU kwa wenye miaka kati ya 15 na 64 ni asilimia 52 lakini kati ya hao, 57.5 ni wanawake na wanaume ni 41.2.

Amesema kwa mujibu wa Mkakati wa Taifa wa Ukimwi unaoishia mwaka huu,gharama za kugharamia Ukimwi nchini zinakadiriwa kufikia Sh6 trilioni kwa muda wa miaka mitano.

Naye waziri wa nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera), Jenista Mhagama amesema mwaka 2015 wafadhili wa tume hiyo walianza kupunguza fedha za mapambano dhidi ya VVU.
Na Sharon Sauwa, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527