SUALA LA MADANGURO NA BIASHARA YA NGONO LAIBUKA BUNGENI

Serikali imesema ina andaa mikakati itakayowezesha kudhibiti biashara ya ngono na uwepo madanguro nchini, hasa kwenye maeneo ya mijini.


Hayo yamesemwa jana Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtambwe, Khalifa Mohammed Issa aliyehoji juu mpango serikali katika kudhibiti biashara ya ngono na madanguro ili kupunguza maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) nchini.


Akijibu swali la Issa, Dkt. Ndugulile alisema Serikali inaandaa mikakati mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu kuhusu madhara ya biashara ya ngono kwa jamii pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa wanaojihusisha na baishara hiyo, pamoja na kudhibiti uwepo wa madanguro.


Katika hatua nyingine, Dkt. Ndugulile alisema serikali inaendelea kuchukua hatua katika kudhibiti mila na desturi potofu zinazochangia maambukizi mapya ya VVU, ikiwemo ukeketaji na urithishaji wa wajane kwa ndugu wa mume, kwa kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya mila potofu pamoja na kutoa hamasa kwa wakunga wa jadi wanaojihusisha na ukeketaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527