MENEJA OFISI YA TAKWIMU AAINISHA IDADI YA KAYA ZINAZOFANYIWA UTAFITI WA MATUMIZI YA KAYA BINAFSI 2018/2019 MKOANI MWANZA

Meneja wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu mkoani Mwanza, Goodluck Lyimo amebainisha idadi ya kaya zinazofanyiwa zoezi la utafiti wa Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara 2017/2018 mkoani Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, meneja huyo alisema  zoezi hilo linahusisha jumla ya kaya 408 mkoani Mwanza ambapo tayari Kaya 68 zimekamilisha mahojiano, Kaya 30 zinaendelea na mahojiano na kwamba hadi kufikia februari 28 mwaka huu Kaya 98 zitakuwa zimekamilisha mahojiano hayo. 

"Zoezi hili la utafiti wa Mapato na  Matumizi ya Kaya Binafsi linafanyika nchi nzima, kwa mkoa wa Mwanza tuna zaidi ya maeneo 34 na lilianza tangu Disemba 1, 2017 na litakwenda hadi Novemba 28, 2018, ni zoezi la miezi 12 kwa maana ya mzunguko wa mwaka mzima."

"Madhumuni makubwa ya utafiti huu itaisaidia serikali kupata takwimu sahihi zitakazotumika kwenye kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo" Alisema Lyimo.

Afisa habari kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Emmanuel Gulla alibainisha kwamba utafiti huo ni wa saba kufanyika nchini tangu uhuru na kwamba utafiki wa mwisho ulifanyika mwaka 2011/12 na kuonyesha kuwa asilimia 28.2 ya watanzania wanaishi chini ya mahitaji ya msingi.

Zoezi la utafiti wa Matumizi ya Kaya binafsi 2017/2018 linafanyika kwenye maeneo yapatayo 796 ambapo jumla ya kaya 11,940 chini ya wadadisi wapatao 629 wakiwa chini ya wasimamizi 100 wakiongozwa na mameneja takwimu pamoja na maofisa wengine kutoka ofisi ya Taifa ya takwimu.
Theme images by rion819. Powered by Blogger.