MANAIBU WAZIRI, MAVUNDE NA BITEKO WAFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA MGODI WA ALMASI EL - HILAL KISHAPU SHINYANGA

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Mhe. Antony Mavunde, na Naibu Waziri Madini Mhe. Dotto Biteko, leo Jumanne Februari 27,2018 wamefanya ziara ya kushtukiza kwenye mgodi wa almasi wa El – Hilal Minerals Limited uliopo katika kijiji cha Maganzo kata ya Maganzo wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga. 

Manaibu Waziri hao walikuwa wameambatana na maafisa kutoka WCF na Ofisi ya Kazi ,lengo la ziara hiyo ikiwa ni kubaini kama wamiliki wa mgodi huo wanatekeleza sheria za uendeshaji. 

Wakati Mheshimiwa Mavunde alikuwa akifuatilia kama mgodi huo umejisajili na Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi (Workers Compensation Fund -WCF), Mhe. Biteko alikuwa akifuatilia kwa nini mgodi huo haujawasilisha wizarani mpango wa ukarabati wa mazingira (rehabilitation plan) na mpango wa uwajibikaji wa shirika kwa jamii (Corporate Social Responsibility-CSR). 

Akiwa katika mgodi huo Mhe. Mavunde alibaini kuwa Mgodi huo bado ulikuwa haujajisajili na Mfuko wa WCF na badala yake uongozi ulipeleka michango siku moja kabla ya ziara ya Naibu waziri huyo kufika katika mgodi huo. 

“Serikali inataka waajiri wazingatie sheria, na ninyi mmevunja sheria kwa kutojisajili, ingawa mmelipa michango yenu jana, ninachoweza kusema, agizo la serikali la kuwafikisha mahakamani waajiri ambao hawajajisajili nchi nzima liko pale pale, ni juu yenu kutekeleza hilo kabla hamjapelekwa mahakamani”, alisema Mhe. Mavunde. 

Mhe. Mavunde pia alibaini kuwa mgodi huo hautoi mikataba ya kudumu kwa wafanyakazi,wafanyakazi kufanyishwa kazi zaidi ya muda wa kazi bila malipo,wafanyakazi kutopewa vifaa kinga na mishahara kutolipwa kwa wakati na kuwaagiza kurekebisha mapungufu yaliyopo kwenye mgodi huo ndani ya siku 30. 

“Nawapa siku 14 za kujisajili WCF na kurekebisha mapungufu yaliyopo hapa ndani ya siku 30,ni lazima tutii na kuziheshimu sheria zetu wanaokiuka sheria tunawafikisha mahamani”,alisema Mhe. Mavunde. 

Ziara ya Naibu Waziri Mavunde ni muendelezo wa ziara yake iliyoanza Februari 26, 2018 jijini Mwanza ambapo aliagiza kufikishwa mahakamani waajiri watatu jijini Mwanza ambao hawajajisajili katika mfuko wa WCF. 

Mhe. Mavunde ameagiza waajiri hao kufanya mawasiliano na watendaji wa Mfuko haraka iwezekanavyo ili kuweza kubaini kiwango cha riba kila mwajiri anachopaswa kulipa kutokana na kuchelewesha michango katika Mfuko. 

“Ni kosa la jinai kwa mwajiri kutotekelza takwa hilo la kisheria na kifungu cha 71(4) cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi kimeweka wazi kuwa mwajiri wa aina hii, anaweza kutozwa faini isiyozidi shilingi milioni 50,000, kifungo kisichozidi miaka 5 jela au adhabu zote kwa pamoja,Nitoe wito kwa waajiri hao, hakuna sababu ya kushurutishwa kutekeleza sheria­”,alisema Mhe. Mavunde.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Mhe. Antony Mavunde akizungumza katika mgodi wa almasi wa El - Hilal Minerals Ltd leo Februari 27,2018 akifuatilia kama mgodi huo umejisajili na Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi -WCF. Aliutaka mgodi huo kuzingatia sheria za nchi la sivyo watawafikisha makahamani. Kulia ni Naibu Waziri Madini Mhe. Dotto Biteko. Kushoto ni Meneja Rasilimali Watu wa Mgodi huo,Gofrey Leshange. Picha zote na Kadama Malunde- Malunde1 blog
Kulia ni Naibu Waziri Madini Mhe. Dotto Biteko akielezea namna mgodi huo unavyokiuka sheria na kuwataka kuwasilisha wizarani mpango wa ukarabati wa mazingira (rehabilitation plan) na mpango wa uwajibikaji wa shirika kwa jamii (Corporate Social Responsibility-CSR). 
Katikati ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Mhe. Antony Mavunde akiangalia mikataba ya wafanyakazi katika mgodi huo ambapo alibaini kuwa mgodi huo hautoi mikataba ya kudumu kwa wafanyakazi na kuwataka kurekebisha mapungufu hayo ndani ya siku 30.
Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano WCF ,Laura Kunenge na Kamishna wa Kazi Msaidizi nchini Rehema Moyo wakiangalia mikataba ya wafanyakazi katika mgodi huo na kubaini kuwa kuna ukiukwaji wa sheria. Aliyesimama ni Afisa Kazi Mfawidhi mkoa wa Shinyanga,Revocatus Mabula.
Wa pili kushoto ni Meneja Rasilimali Watu wa Mgodi huo,Gofrey Leshange akijitetea kwanini hawatoi mikataba ya kudumu kwa wafanyakazi wao na badala yake wanatoa mikataba ya miezi sita hadi mwaka mmoja.
Mazungumza yakiendelea katika mgodi huo.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Mhe. Antony Mavunde na Naibu Waziri Madini Mhe. Dotto Biteko wakielekea katika eneo la uzalishaji wa almasi katika mgodi wa El - Hilal uliopo Kishapu mkoani Shinyanga
Kushoto ni Meneja Rasilimali Watu wa Mgodi huo,Gofrey Leshange akielezea namna uzalishaji wa almasi unavyofanyika katika mgodi huo
Mfanyakazi wa mgodi huo "Plant Manager",Peter Mayeka akielezea jambo 
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Mhe. Antony Mavunde na Naibu Waziri Madini Mhe. Dotto Biteko  wakitoka katika chumba cha kuhifadhi almasi katika mgodi wa El - Hilal
Mwenyekiti wa wafanyakazi katika mgodi wa almasi wa El - Hilal Evarist Seleman akielezea changamoto zilizopo katika mgodi huo.
Kushoto ni Mhasibu katika mgodi wa El- Hilal Amour Nassor akijitetea baada ya wafanyakazi wa mgodi huo kuwaeleza manaibu Waziri hao kuwa mgodi huwa haulipi Overtime na mishahara kucheleweshwa.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Mhe. Antony Mavunde na Naibu Waziri Madini Mhe. Dotto Biteko wakisaini vitabu vya wageni katika ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Shinyanga baada ya kuwasili mkoani Shinyanga kueleza lengo la ziara yao. Katikati ni Katibu wa CCM mkoa wa Shinyanga, Haula Kachwamba
Naibu Waziri Madini Mhe. Dotto Biteko akizungumza katika ofisi ya Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga walipowasili mkoani Shinyanga kuueleza uongozi wa mkoa lengo la ziara yao.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Mhe. Antony Mavunde akielezea zaidi kuhusu  ziara yake na mwenzake mkoani Shinyanga.
Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga, Dk. Rashid Mfaume akisoma taarifa ya mkoa kwa manaibu waziri hao.
Afisa Kazi Mfawidhi mkoa wa Shinyanga,Revocatus Mabula akizungumza.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Mhe. Antony Mavunde akimweleza mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro (kulia) lengo la ziara yao.
Naibu Waziri Madini Mhe. Dotto Biteko akizungumza katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Shinyanga (Josephine Matiro - kulia).
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527