MWANAFUNZI KIONGOZI WA CHUO KIKUU AUAWA KWA KUPIGWA RISASI NA POLISI

 Evans Njoroge
Kifo cha Mwanafunzi wa Chuo kikuu nchini Kenya kimezua shutuma mpya za mauaji yanayodaiwa kutekelezwa na maafisa wa polisi nchini humo.


Ripoti zinasema Evans Njoroge, mwanafunzi ambaye alikuwa kiongozi Chuo kikuu cha Meru nchini humo, aliuawa kwa kupigwa risasi na anayedaiwa kuwa polisi.

Mwandishi wa BBC, Ferdinand Omondi anasema picha za mwili wa kijana huyo, damu yake ikionekana imetapakaa kote, zimekuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii huku raia wa Kenya wakighadhabishwa na kile walichodai kuwa mauaji yanayotekelezwa na polisi.

Evans alipigwa risasi Jumanne wakati wa maandamano ya wanafunzi waliokuwa wakilalamikia ongezeko la ada dhidi ya chuo cha Meru.

Vyombo vya habari nchini Kenya vimemnukuu shuhuda mmoja akisema polisi walimkimbiza Evans wakamfikia kisha mmoja wao akampiga risasi na kuondoka.

Mkuu wa polisi Jenerali Joseph Boinnet ameamuru kufanyika uchunguzi kuhusu kifo hicho baada ya kuwepo kwa wanasiasa na makundi ya wanaharakati waliokuwa wakitaka mauaji yanayodaiwa kutekelezwa na polisi kukoma mara moja.

Shirika huru la kiraia linalofuatilia shughuli za polisi (IPOA) limesema limewatuma maafisa wake kuchunguza tukio hilo.

Mwanafunzi huyo aliuawa katika eneo la Nchiru, eneo la Tigania West katika jimbo la Meru ambalo linapatikana katika eneo la Mlima Kenya.

IPOA wamesema maafisa wa uchunguzi wametukwa kwa lengo la: "kuchunguza kuhusu yaliyotokea wakati wa mauaji hayo na iwapo kuna mtu anayefaa kulaumiwa, na kuhakikisha afisa yeyote wa polisi atakayepatikana na hatia anawajibishwa kisheria."

Wakenya mtandaoni wamekuwa wakishutumu mauaji hayo.

Shutuma hizi mpya zimekuja siku kadhaa baada ya shirika linalotetea haki za binadamu la Human Rights Watch kuwasilisha ushahidi mpya kuwa polisi nchini Kenya waliua watu takriban 23 wakati wa kipindi cha marudio ya uchaguzi nchini humo mwaka jana.

Kwa mujibu wa ripoti,uchunguzi umebaini kuwa wengi wa waathirika walifyatuliwa risasi na silaha za nguvu.

Polisi wameendelea kukana shutuma hizo.

Chanzo - BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post