RAIS MAGUFULI ATAJA SABABU ZA KUMUUNGA MKONO KAGAME KUONGOZA UMOJA WA AFRIKA (AU)

Rais John Magufuli amesema Rais Paul Kagame wa Rwanda anafaa kuongoza Umoja wa Afrika (AU) kwa sababu ya historia yake na hivyo anazifahamu changamoto zinazolikabili bara hili.


Rais Magufuli alisema hayo jana Ikulu wakati Kagame alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja, ikiwa ni mara yake ya pili kufanya ziara tangu Rais Magufuli alipoapishwa. Alifanya ziara kwa mara ya kwanza Julai Mosi, 2016.


Magufuli alimwaga sifa hizo akianzia matatizo yaliyoibuka nchini Libya baada ya kiongozi wake wa kijeshi, Muamar Gadaffi kuondolewa madarakani kwa vurugu licha ya kuliongoza taifa hilo vizuri kiuchumi.


“Baada ya kiongozi wa Libya kuondoka, na nyinyi nyote mnajua, matokeo yake ni haya. Na haya ndiyo ya ukweli na utabaki kuwa ukweli,” alisema Rais Magufuli katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jana.


“Nina uhakika Mheshimiwa Kagame atakapokuwa mwenyekiti wetu Afrika, atayaadress (atayashughulikia haya), atayaadress vizuri masuala ya migogoro miongoni mwa nchi za Afrika, atayaaddress vizuri masuala ya ukoloni mamboleo unaoweza kuletwa na mtu yeyote kutoka nje akasababisha matatizo kwa Waafrika.


“Mheshimiwa Kagame hadi kufikia urais anafahamu shida za wananchi wa Rwanda; anajua historia ya Rwanda ilitokotoka hadi ikatokea genocide (mauaji ya watu wengi). Anafahamu mateso ya Wanyarwanda; anafahamu mateso yanayoweza kuletwa na mtu hata mmoja tu, inawezekana ikawa ni media kwa kutangaza au kuandika kitu cha ovyo kikaleta multiplying effect.”


Alisema ndio maana anaamini kutokana na mchango wake kwa Afrika na kwa sababu ni mwanamapinduzi mzuri, uzoefu wake utasaidia maendeleo ya Afrika.


“Rais Kagame ni mwanamapinduzi wa kweli wa Afrika, ameishi maisha ya Kiafrika, maisha ya mateso tangu akiwa kijana; ameishi kwenye nchi za ugenini kama mkimbizi, anayafahamu mateso ya kijana,” alisema.


“Kwa hiyo kwa yale maisha aliyoyaishi kama mkimbizi, kama kijana, nina uhakika ataleta mageuzi makubwa Rwanda ambayo ameshaanza kuyaleta, lakini ataleta mageuzi makubwa Afrika.”


Alisema Tanzania inamuunga mkono Rais Kagame kwa nguvu zote ili kuwepo kwa mabadiliko ya kiuchumi kwa Waafrika wote hasa kwa vijana ambao ndiyo nguvu kazi kubwa katika bara hili.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527