RAIS KAGAME AWASILI TANZANIA ZIARA YA SIKU MOJA


Rais wa Rwanda, Paul Kagame amewasili nchini leo Januari 14 kwa ziara ya siku moja na kupokelewa na mwenyeji wake, Rais John Magufuli.

Baada ya kuwasili katika uwanja wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA), Rais Kagame alielekea katika chumba maalumu na kukaa hapo kwa takribani dakika 30.

Aliondoka uwanjani hapo saa 4:45 na kuelekea Ikulu ambapo atafanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Magufuli.

Hii ni mara ya pili kwa Kagame kuwasili nchini na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli tangu mwaka 2015. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2016 ambapo alifanya ziara na kushiriki maonesho ya 40 ya biashara (Sabasaba).
Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame leo tarehe 14 Januari, 2018 amefanya ziara ya kikazi ya siku moja hapa nchini kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

Mhe. Rais Kagame amewasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kupokelewa na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli na kisha kulakiwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, na baadaye akaelekea Ikulu ambako pamoja na kufanya mazungumzo ya faragha, viongozi hao wamezungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari.

Mhe. Rais Magufuli amesema katika mazungumzo yao wamekubaliana ujenzi wa reli kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kati ya Isaka nchini Tanzania na Kigali nchini Rwanda yenye urefu wa takribani kilometa 400 uanze mwaka huu (2018), na wamewaagiza Mawaziri wanaohusika na miundombinu kukutana ndani ya kipindi cha wiki mbili kuanza sasa ili kuweka mipango ya utekelezaji ikiwemo upatikanaji wa fedha.

Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa wakati uamuzi huo ukifikiwa, Tanzania ambayo tayari imeanza ujenzi wa reli ya kati (Standard Gauge) kuanzia Dar es Salaam – Morogoro hadi Dodoma yenye urefu wa kilometa 726 na itakayogharimu Shilingi Trilioni 7.6, itaanza mchakato wa kuunganisha sehemu iliyobaki ya kutoka Dodoma – Isaka yenye urefu wa takribani kilometa 400 ili mizigo iweze kusafirishwa moja kwa moja kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi Kigali nchini Rwanda.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa japo kuwa kumekuwa na ongezeko la mizigo ya Rwanda inayosafirishwa kupitia Tanzania iliyofikia tani 950,000 kwa mwaka, biashara kati ya nchi hizi mbili sio ya kuridhisha na hivyo amesema wamekubaliana kuboresha zaidi mazingira ya biashara ikiwemo kuimarisha miundombinu ya reli na barabara na kuwahamasisha wafanyabiashara wa Tanzania na Rwanda kufanya biashara zaidi.

“Tukijenga reli kutoka Isaka hadi Kigali, na sisi huku tunajenga kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na tukaunganisha Dodoma hadi Isaka, mizigo mingi ya Rwanda itasafirishwa kupitia bandari ya Dar es Salaam, biashara itakua zaidi na ajira zitaongezeka, kule Lulenge Ngara, Burundi na Rwanda kote kuna madini ya Nickel, tukijenga miundombinu yetu tutasafirisha madini haya na tutaongeza biashara.

“Na reli hii itatumiwa na nchi nyingine za Burundi, DRC na Uganda, kwa hiyo ni jambo muhimu sana kwa uchumi wetu na majirani” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia Mhe. Rais Kagame kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Rwanda kwa manufaa ya wananchi, na kwamba ipo tayari kumuunga mkono atakapochaguliwa kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) katika kikao cha wakuu wa nchi na Serikali kinachotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu wa Januari, 2018 Mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.

“Mhe. Rais Kagame nakupongeza sana, unafanya kazi kubwa ya kuwapigania wananchi wako, Watanzania tunajua ulikoitoa Rwanda na tunajua ulipoifikisha, nakuhakikishia tutaendelea kushirikiana katika jukumu la kuwaletea wananchi maendeleo” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Kwa upande wake Mhe. Rais Kagame amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa mwaliko wake na amempongeza kwa kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi yake na Tanzania.

Mhe. Rais Kagame amesema yeye na Mhe. Rais Magufuli wameamua kufanya kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo na ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na Mhe. Rais Magufuli ili mipango yote waliyojiwekea itekelezwe ikiwemo kuinua biashara na kuongeza ajira, na pia ameshukuru kwa Tanzania kuwa tayari kumuunga mkono atakapochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa AU.

Mhe. Rais Kagame amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku moja hapa nchini na amerejea nchini kwake Rwanda.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

14 Januari, 2018

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527