Picha : AGAPE YAKUTANA NA WANAFUNZI VIONGOZI NA WALIMU WALEZI DIDIA KUWEKA MIKAKATI KUZUIA MIMBA NA NDOA ZA UTOTONI

Shirika lisilo la kiserikali la Agape AIDS Control Programme (AACP) la Mjini Shinyanga limekutana na wanafunzi viongozi wa klabu za 'Tuseme' shuleni, walimu walezi na baadhi ya viongozi wa kata ya Didia iliyopo halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ili kuweka mikakati ya kuzua ndoa na mimba za utotoni katika kata ya Didia.


Kikao hicho kimefanyika leo Ijumaa Januari 19,2018 katika shule ya msingi Didia na kukutanisha wanafunzi viongozi wa klabu shuleni na walimu walezi kutoka shule za msingi Didia,Mwanono,Bugisi,Mwamalulu ,Bukumbi na shule ya Sekondari Didia.

Akizungumza katika kikao hicho,Meneja Mradi wa Kuzuia mimba na ndoa za utotoni kutoka shirika la AGAPE,Mustapha Isabuda alisema lengo la kikao hicho ni kuweka mikakati ya kuzuia mimba na ndoa za utotoni katika kata hiyo ili wanafunzi waweze kumaliza masomo yao vizuri.

Alisema wanafunzi hao watakuwa mabalozi katika mapambano dhidi ya ndoa na mimba za utotoni kupitia klabu za “Tuseme”  kwa ajili ya kuzuia mimba na ndoa za utotoni.

“Klabu hizi zinasimamiwa na walimu walezi ambapo wanafunzi huwa wanapeana elimu kuhusu namna ya kuzuia mimba na ndoa za utotoni na masuala mengine ya ukatili dhidi ya watoto,na watakuwa mabalozi kuielimisha jamii juu ya haki za watoto na madhara ya ukatili dhidi ya watoto”,alieleza Isabuda.

“Hatutaki kuona mwanafunzi anakatiza masomo kwa sababu ya kupewa mimba ama kuolewa, ni wajibu wetu wanafunzi,walimu,serikali na wadau wote tushirikiane kupaza sauti ili watoto wetu watimize ndoto zao”,alieleza Isabuda.

Isabuda alisema pamoja na mafanikio yaliyofikiwa na shirika la AGAPE katika mapambano dhidi ya mimba na ndoa za utotoni,shirika hilo limekuwa likitoa elimu kwa wanafunzi,walimu na viongozi mbalimbali katika jamii.

Kwa upande wake,Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGAPE John Myola alisema bado jitihada kubwa zinatakiwa kufanyika ili kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto katika jamii kwani baadhi ya matukio yamekuwa yakifanywa na ndugu wa karibu.

“Watoto wamekuwa wakibakwa na ndugu na watu wa karibu,lakini pia baadhi ya watendaji wa serikali siyo waaminifu kwani wamekuwa wakizifanya dili hizi kesi za watoto hivyo lazima wadau wote wapaze sauti na kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria”,alieleza Myola.

Aidha aliwataka walimu kutunza siri za wanafunzi na kutopuuza taarifa wanazopewa na wanafunzi kuhusu vitendo vya ukatili wanavyokutana navyo.

Naye Secilia Kiza kutoka dawati la jinsia na watoto jeshi la polisi wilaya ya Shinyanga aliwataka wanafunzi kutofumbia macho vitendo vya ukatili na watoe taarifa katika vyombo vinavyotakiwa.

Nao walimu na wanafunzi waliohudhuria kikao hicho waliahidi kutoa elimu ya namna ya kuzuia mimba na ndoa za utotoni katika shule zao na jamii kwa ujumla ili kuhakikisha matukio hayo yanakomeshwa mkoani Shinyanga.
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGAPE,John Myola akizungumza katika kikao chao na wanafunzi na walimu kutoka shule za msingi Didia,Mwanono,Bugisi,Mwamalulu ,Bukumbi na shule ya Sekondari Didia zilizopo katika kata ya Didia halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kilichofanyika katika shule ya msingi Didia leo Ijumaa Januari 19,2018 - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGAPE John Myola akizungumza katika kikao hicho ambapo aliwataka wanafunzi kufichua vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na walimu kuwa wadadisi wa mambo mbalimbali wanayoambiwa na wanafunzi wao.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGAPE John Myola pia aliwasisitiza wanafunzi kuepuka vishawishi ili waweze kumaliza masomo yao vizuri
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGAPE ,John Myola akizungumza wakati wa kikao hicho
Meneja Mradi wa Kuzuia mimba na ndoa za utotoni kutoka shirika la AGAPE,Mustapha Isabuda akielezea lengo la kukutana na wanafunzi na walimu kwa ajili ya kujadili namna ya kuzuia mimba na ndoa za utotoni
Meneja Mradi wa Kuzuia mimba na ndoa za utotoni kutoka shirika la AGAPE,Mustapha Isabuda akizungumza katika kikao hicho ambapo alisema matukio ya mimba na ndoa za utotoni yamepungua mkoani Shinyanga kutoka asilimia 59 hadi 34 kutokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na wadau.
Meneja Mradi wa Kuzuia mimba na ndoa za utotoni kutoka shirika la AGAPE,Mustapha Isabuda akionesha picha ya watoto waliosaidiwa na shirika la AGAPE baada ya watoto hao kukatishwa masomo kwa kupewa ujauzito na wengine kuolewa wakiwa na umri mdogo
Meneja Mradi wa Kuzuia mimba na ndoa za utotoni kutoka shirika la AGAPE,Mustapha Isabuda akiendelea kuonesha picha
Walimu na wanafunzi wakiwa wameshikana mikono ishara ya kwamba wapo tayari kuzuia mimba na ndoa za utotoni
Secilia Kiza kutoka dawati la jinsia na watoto jeshi la polisi wilaya ya Shinyanga akizungumza katika kikao hicho ambapo aliwasisitiza wanafunzi,walimu na jamii kwa ujumla kutoa taarifa pale wanapoona kuna matukio ya ukatili dhidi ya watoto.
Secilia Kiza kutoka dawati la jinsia na watoto jeshi la polisi wilaya ya Shinyanga akitoa elimu kuhusu masuala ya ukatili.
Kaimu Afisa Mtendaji wa kata ya Didia,William Nkuya akizungumza katika kikao hicho ambapo alisisitiza umuhimu wa wadau kushirikiana ili kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
Mwalimu Bertha Msengwa kutoka shule ya Sekondari Didia akizungumza kwa niaba ya walimu waliohudhuria kikao hicho ambapo alisema wapo tayari kuzuia ndoa na mimba za utotoni.
Mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya sekondari Didia,Hellena Mussa akizungumza katika kikao hicho ambapo alisema wataenda kutoa elimu ya namna ya kuzuia mimba na ndoa za utotoni
Picha ya pamoja washiriki wa kikao hicho
Picha ya pamoja.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527