NYOSSO ASHTAKIWA KWA KUMPIGA SHABIKI



Baada ya mchezaji Juma Nyosso wa Kagera Sugar kumpiga shabiki, kamati ya usimamizi na uendeshaji wa ligi imemshitaki kwenye kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya hatua zaidi.

Akiongea leo Afisa Mtendaji mkuu wa Bodi ya ligi Boniface Wambura amesema kamati hiyo imepitia ripoti ya kamishna wa mchezo huo namba 112 kati ya Kagera Sugar dhidi ya Simba SC na kubaini kuwa tukio hilo ni la kinidhamu hivyo kulifikisha sehemu husika.

''Kamati imepitia ripoti ya kamishna na imeonesha kuwa kulikuwa na tukio ambapo mchezaji wa Kagera Sugar Juma Nyosso alimpiga ngumi shabiki hivyo suala hilo limefikishwa kwenye kamati ya nidhamu ya TFF kwa ajili ya maamuzi'', amesema Wambura.

Nyosso ambaye bado anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Kagera anatuhumiwa kwa kumpiga ngumi shabiki baada ya mchezo kumalizika, kitendo ambacho kilipelekea shabiki huyo kuanguka na kuzimia kabla ya kukimbizwa Hospitali.

Katika mchezo huo uliopigwa Jumatatu Januari 22 Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 na kulipa kisasi cha msimu uliopita ambapo ilipoteza 2-1 kwenye mchezo uliopigwa April 22, 2017.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527