BOT YAKUNJUA MAKUCHA KWA BENKI 'KOROFI'….YAFUTA BENKI TANO

Benki Kuu ya Tanzania(BoT) imezifutia leseni ya kufanya biashara benki tano na kuziweka chini ya ufilisi.


Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi na BoT imezitaja benki hizo kuwa ni Covenant Bank For Women (Tanzania) Limited, Efatha Bank Limited, Njombe Community Bank Limited, Kagera Farmers' Cooperative Bank Limited, na

Meru Community Bank Limited.

BoT imeeleza kuwa imefanya hivyo kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu cha 56(1)(g), 56(2) (a), (b) na (d), 58(2)(i), 11(3)(c) na (j), 61(1) na 41(a) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu ya Tanzania imeamua kuzifunga; kusitisha shughuli zake zote za kibenki; kufuta leseni zake za biashara ya kibenki; na kuziweka chini ya ufilisi.

“Kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu Na. 41(a) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006; Benki Kuu ya Tanzania imeiteua Bodi ya Bima ya Amana (The DEPOSIT INSURANCE BOARD) kuwa mfiiisi kuanzia tarehe 04 Januari 2018,” imeeleza taarifa hiyo.”

“Uamuzi huu umechukuliwa baada ya Benki Kuu ya Tanzania kujiridhisha kuwa benki hizi zina upungufu mkubwa wa mtaji kinyume na matakwa ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake. Upungufu huo wa mtaji unahatarisha usalama wa sekta ya fedha na kwamba kuendelea kutoa huduma za kibenki kwa benki hizo kunahatarisha usalama wa amana za wateja wake.”

Taarifa hiyo imeeleza kuwa BoT inapenda kuuhakikishia umma kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la kuleta uhimilivu katika sekta ya fedha.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527