Thursday, December 28, 2017

VIONGOZI WA UMMA WATAKIWA KUKABIDHI ORODHA YA MALI ZAO KABLA YA DESEMBA 31

  Malunde       Thursday, December 28, 2017
Kamishna wa Maadili, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu Harold Nsekela amewahimiza Viongozi wa Umma kukamilisha taratibu za ujazaji wa fomu za tamko la rasilimali na madeni kabla ya Disemba 31 mwaka huu.


Ametoa kauli hiyo jana Jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inayomtaka kiongozi wa umma kupeleka tamko kwa maandishi lililo katika hati rasmi linaloorodhesha mali au rasilimali za kiongozi na familia yake kwa Kamishna wa Maadili kila mwisho wa mwaka.


Jaji Mstaafu Nsekela amesema kuwa fomu za tamko hilo zinapatikana kwenye tovuti ya Sekretarieti ya maadili ambayo ni www.ethicssecretariat.go.tz hivyo ametoa wito kwa viongozi ambao hadi sasa hawajapata fomu kutumia tovuti hiyo kupata fomu kwa urahisi.


“Kwa kuzingatia kifungu cha 9 (1) (a) na (c) cha Sheria na Maadili ya Viongozi wa Umma, viongozi wapya wanaochaguliwa au kuteuliwa wanatakiwa kujaza fomu hizi ndani ya siku thelathini baada ya kupewa wadhifa fulani pia anapofika mwisho wa kutumikia wadhifa huo anapaswa kujaza fomu na kuzirejesha katika ofisi yetu,” alisema Jaji Mstaafu Nsekela.


Jaji Mstaafu Nsekela amefafanua kuwa fomu hizo zinatakiwa kuwasilishwa katika Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa Umma zilizopo Jijini Dar es Salaam au katika ofisi zao za Kanda zilizopo katika Mikoa ya Dodoma, Mwanza, Arusha, Mtwara, Tabora, Pwani na Mbeya.


Kwa upande wake Afisa Sheria Mkuu wa Sekretarieti hiyo, Filotheus Manula amesema kuwa kujaza fomu hizo ni takwa la kikatiba hivyo Viongozi wa Umma wahakikishe wanajaza fomu hizo bila kudanganya.


“Ni kosa kwa mujibu wa Kifungu cha 15(c) cha Sheria za Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kiongozi kushindwa kutoa tamko bila sababu ya msingi kwani sheria hizi hazimzuii kiongozi kumiliki au kuwa na mali nyingi bali mali hizo zinatakiwa kutolewa maelezo ya chanzo cha upatikanaji wake,” alisema Manula.


Aidha, Manula amefafanua kuwa kosa hilo linaweza kumpelekea muhusika kuonywa au kupewa adhabu ya kushushwa cheo, kusimamishwa, kufukuzwa kazi pamoja na kupelekwa Mahakamani.


Vile vile Manula amesema kuwa kwa sasa hali ya uadilifu kwa Viongozi wa Umma inaridhisha kwani ukiukwaji wa maadili umepungua kwa kiasi kikubwa.
Na Jacquiline Mrisho
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post