ASKOFU KAKOBE KUHOJIWA NA POLISI MANENO YA KASHFA

Licha  ya kutokiri moja kwa moja juu ya taarifa zinazosambaa mitandaoni kuhusu kumkamata Askofu Zakaria Kakobe wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGFC) lililoko Mwenge jijini Dar es Salaam, Jeshi la Polisi limesema ni lazima litamhoji kiongozi huyo wa kiroho.

Kuhojiwa huko kumetokana na kauli yake dhidi ya serikali aliyoitoa wakati wa ibada ya Krismasi.

Jana, kulienea taarifa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kueleza kwamba askofu huyo alitiwa mbaroni jana asubuhi na askari wa Jeshi la Polisi huku sababu za kukamatwa zikielezwa kuwa ni ujumbe alioutoa wakati wa mahubiri yake ya ibada ya Krismasi.

Akizungumza na Nipashe jana kuhusiana na ukweli wa taarifa za kutiwa mbaroni kwa Askofu Kakobe, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema kuwa ni kweli walishakuwa katika harakati za kumkamata.

"Ametoa maneno ya kashfa katika mahubiri yake, lakini sina taarifa kama amekamatwa," Kamanda Mambosasa alisema na kuongeza:

"Taarifa za kumkamata zipo, lazima tumkamate. Tutamhoji…tutamhoji alikuwa na maana gani.

“Mtu akitenda kosa la jinai ni lazima akamatwe…kwa sasa niko msibani, sijapokea taarifa kama amekamatwa au kuhojiwa. Nitawaarifu kama kutakuwa na taarifa zaidi.”

Askofu Kakobe (62), anadaiwa kuyatumia mahubiri yake siku hiyo kuzungumzia mwenendo wa serikali na masuala mbalimbali ya kisiasa nchini.

Mojawapo ya sauti inayodaiwa kuwa ya Askofu Kakobe na kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ilidai kwamba hivi sasa Tanzania si nchi ya chama kimoja kama viongozi wanavyotaka.

Chanzo: Nipashe

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527