RAIS MAGUFULI AAHIDI KULIPA MADENI YA WALIMU

Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameahidi kulipa madeni ya walimu takribani shilingi Bil. 25 mara baada ya viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kuthibitisha uhalali wa madeni hayo.


Rais Dkt. Magufuli ametoa tamko hilo jana Mjini Dodoma ,alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa CWT ambao umehusisha wawakilishi kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara .
“Ninawaahidi walimu wenzangu, mara baada ya zoezi la uhakiki kuisha wale walimu ambao wanadai malipo halali watalipwa,”alifafanua Rais Dkt. Magufuli.

Aliendelea kusema kuwa kabla hajawa Rais alikuwa mwalimu hivyo anazifahamu vizuri shida za walimu hivyo walimu wajisikie wana muwakilishi mzuri.

Aidha, Rais Magufuli amewataka viongozi wa CWT wa wilaya na mikoa kuhakiki madeni ya walimu ya maeneo yao na kuyawasilisha kwa Waziri Mkuu kwa ajili ya kulipwa.


Rais Dkt. Magufuli amesema Serikali ya awamu ya Tano imeendelea kufanya jitihada za kuboresha maslahi ya walimu ambapo tangu imeingia madarakani jumla ya shilingi bilioni 56.92 zimetolewa kwa ajili ya kulipa madeni ya walimu ambapo kati ya fedha hizop, shilingi bilioni 14.23 ni madeni ya mishahara na shilingi bilioni 42.69 ni madeni yasiyo ya mishahara.


Vile vile Rais Magufuli amewasihi walimu wenzake kupokea kile kidogo ambacho Serikali inakitoa wakati huu ambapo Serikali inawekeza katika kutekeleza miradi mbalimbali kama vile miradi ya afya, umeme, maji, barabara na reli. Miradi ambayo inawagusa pia walimu katika maisha yao ya kila siku nawanapotimiza majukumu yao.


Wakati huo huo, Rais Magufuli amewaahidi walimu hao kufanyia kazi maombi mbalimbali ambayo wamewasilisha ikiwemo kurudisha posho ya kufundishia pamoja na Serikali kutoa mikopo isiyo na riba ili kuwasaidia kujenga nyumba za kuishi.

Hata hivyo, amewata viongozi husika kushughulikia uwiano sahihi wa walimu wa shule za msingi na sekondari walioko mijini na vijijini kutokana na walimu wengi kupangiwa mijini.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais CWT Leah Ulaya alisema kuwa wanaimani na Rais Magufuli na juhudi zake zinaonekana wazi katika kupambana na ufisadi, uzembe, rushwa, uhujumu uchumi na vita dhidi ya madawa ya kulevya.
Na Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527