Picha : DC SHINYANGA ALA CHAKULA CHA PAMOJA NA WATU WANAOISHI KATIKA MAZINGIRA MAGUMU... AGAWA NGUO,VIFAA VYA SHULE


Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro leo Jumatano Desemba 20,2017 amekula chakula cha pamoja na watu wanaoishi katika mazingira magumu katika kata ya Kitangiri manispaa ya Shinyanga pamoja na kutoa msaada wa nguo kwa wazee na vifaa vya shule kwa watoto kwa lengo la kuwafariji na kutambua serikali yao inawajali.

Jumla ya watu wanaoishi katika mazingira magumu waliokula chakula cha pamoja ni 229 kati yao watu wazima ni 117 na watoto 112  ikiwa ni sehemu ya kufurahia nao pamoja sherehe za mwisho wa mwaka ikiwemo Krismasi na Mwaka mpya kama watu wengine wenye uwezo wanavyofurahia katika familia zao.

Akizungumza kwenye hafla hiyo fupi iliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Kitangili, Matiro alisema serikali inataka watu wote waishi kwa amani,upendo na furaha bila ya kujali uwezo wao wa kimaisha na ndiyo sababu kuu iliyosababisha atoe msaada huo, kwa kushirikiana na shirika la PAWWCO.

“Nalipongeza Shirika hili la PAWWCO kwa kushirikiana na serikali kuwafariji watu hawa kula nao chakula pamoja na kutoa msaada wa nguo, sabuni,mafuta ya kupaka ili kuwafanya washeherekee sikukuu za mwisho wa mwaka kwa furaha bila ya kujiona wanyonge”,alisema Matiro.

Alitumia fursa hiyo kuwataka wazazi ambao wametelekeza watoto wao kwa bibi zao waache tabia ya kuwaachia mzigo wazee hao, bali wawahudumie na kama wameshindwa warudi kuwachukua na siyo kuwatesa wazee ambao nao hawana uwezo wa kuwalea na kuwafanya watoto hao kukosa haki zao za msingi.

Naye mratibu wa miradi kutoka shirika la PAWWCO Venny Raymond ambao wanajihusisha na masuala ya jamii, alisema kutokana na wao kuwa karibu na jamii hivyo walikaa na kujadili namna ya kuwafariji watu wanaoishi katika mazingira magumu katika sikukuu za mwisho wa mwaka na kuamua kushirikiana na serikali kutoa msaada huo pamoja na kula nao chakula.

Alisema baada ya kubaini idadi kubwa ya watoto katika kata ya Kitangili wanaishi katika mazingira magumu mara baada ya kutelekezwa na wazazi wao sababu ya kushindwa kuwahudumia na kubaini chanzo chake ni mimba na ndoa za utotoni hivyo wameutambulisha mradi ambao utatokomeza vitendo hivyo ndani mwaka mmoja.

“Mradi huu wa kutokomeza mimba na ndoa za utotoni utadumu ndani ya mwaka mmoja katika kata ya Kitangili manispaa ya Shinyanga, pamoja na Kata mbili za Shinyanga vijijini ambazo ni Namalongo na Solwa,ili kutokomeza tabia ya watoto kutelekezwa na kukosa haki zao za msingi,”alisema.

Nao watu wasiojiweza Anna Ngassa na Sadiki Kisale waliishukuru Serikali na wadau hao wa maendeleo shirika la PAWWCO, kwa faraja hiyo waliyotoa ambapo pamoja na kuwapatia misaada mbalimbali ikiwemo nguo na vifaa vya wanafunzi wa shule, waliwataka wasichoke kuwasaidia.

Kwa upande wao watoto hao Idd Juma na Halima Gambi walisema wanafurahi kupata vifaa hivyo vya shule ambavyo vitawasaidia katika masomo yao na kuwafanya kusoma kwa bidii ili wapate kutimiza malengo yao na kuja kuwasaidia wazazi wao kimaisha pale watakapopata kazi.

ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akigawa vifaa vya shule kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu kata ya Kitangili manispaa ya Shinyanga leo Jumatano Desemba 20,2017.- Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog
Vifaa vilivyotolewa  kwa ajili ya watu wanaoishi katika mazingira magumu.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro(kulia) na Diwani wa viti maalumu Manispaa ya Shinyanga Mariamu Nyangaka wakipanga sabuni kwa ajili ya kugawa kwa watu hao wanaoishi katika mazingira magumu.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akigawa vifaa vya shule kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu
Matiro akiendelea kugawa vifaa vya shule kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu
Diwani wa viti maalumu Manispaa ya Shinyanga Mariamu Nyangaki akigawa sabuni kwa watu hao wanaoishi katika mazingira magumu katika kata ya Kitangili
Watu wanaoishi katika mazingira magumu wakiwa na nguo walizopewa.
Watu wanaoishi katika mazingira hayo magumu wakiteta jambo baada ya kupokea msaada wa nguo
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akigawa pipi kwa watoto
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akigawa nguo kwa mzee Sadiki Kisale ambaye anaishi katika mazingira magumu.
Viongozi wa dini wakiwa na mdau wa maendeleo.Kushoto ni Mama Wambura ambaye ni msaidizi wa Dispensary ya Golden Grace iliyopo kwenye kata hiyo ya Kitangili.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akichukua chakula kwa ajili ya kujumuika na watu hao wanaoishi katika mazingira magumu kwenye kata ya Kitangili mjini Shinyanga.
Zoezi la kuchukua chakula likiendelea
Watu wanaoishi katika mazingira magumu katika kata hiyo ya Kitangili wakila chakula 
Tunakula chakula....
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza wakati wa hafla hiyo ambapo aliwataka wazazi waliotelekeza watoto kwa wazazi wao (bibi) wawahudumie kama wameshindwa warudi kuwachukua wakaishi nao huko walipo kuliko kuwaachia mzigo wazee.
Mratibu wa miradi kutoka Shirika la Pawwco Venny Raymond akizungumza wakati wa hafla hiyo ambapo alisema shirika hilo linafanya kazi zake kwa kushirikiana na serikali katika kuhakikisha linatatua changamoto zinazoikabili jamii ili kuwafanya waishi kwa furaha,amani na upendo.
Picha zote na Marco Maduhu- Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527