NYUMBA YA MBUNGE WA CHADEMA SILINDE DAVID KUCHOMWA MOTO

Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde amesema siku akitangaza kukihama chama hicho wananchi wajitokeze kuchoma moto nyumba yake pamoja na mali zake zinazofahamika.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Desemba 15, muda mfupi baada ya kusambaa kwa taarifa za kutaka kukihama chama hicho kikuu cha upinzani nchini, Silinde amesema ubunge wa jimbo hilo aliutafuta kwa gharama kubwa.

“Kinachofanyika sasa ni kutaka kutuondoa katika hoja, kuna watu wanasema nitafanya mkutano na waandishi wa habari, mimi nikawajibu kuwa hilo haliwezekani. Siwezi kuhama,” amesema.

Akieleza sababu za kusambazwa kwa ujumbe huo amesema, “Wamesambaza uzushi huu baada ya mimi kuandika katika mitandao ya kijamii kuwa unapopigana vita unahitaji jeshi dogo lenye weledi, yaani unaweza kuwa na idadi kubwa ya wanachama lakini wakawa wasaliti.”

Kuhusu gharama za ubunge wake amesema wapo watu waliopigania ushindi awe mwakilishi wao bungeni huku baadhi kupoteza maisha, kufilisika, kufungwa jela na kwamba hawezi kuwasaliti kwa maslahi yake binafsi.

“Thamani ya ubunge haiwezi kushushwa kama vocha ya simu, kwamba ikiisha unaweza kukwangua nyingine,” amesisitiza.

MWANANCHI
Theme images by rion819. Powered by Blogger.