ALIYEKUWA RAIS WA CHAMA CHA WALIMU GRATIAN MUKOBA ANASWA KWA RUSHWA MKUTANO WA CWT




 
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Dodoma inamshikilia aliyekuwa Rais wa Chama cha Walimu (CWT), Gratian Mukoba kwa tuhuma za kugawa rushwa kwa wajumbe wa chama hicho.


Kamanda wa Takukuru mkoani Dodoma, Emma Kuhanga amethibitisha kushikiliwa kwa Mukoba tangu saa tano asubuhi ya leo Jumamosi Desemba 16,2017.


"Ni kweli tunamshikilia tangu saa tano asubuhi, tunaendelea na uchunguzi na kama usipokamilika atalala," amesema.


Kuhanga amesema Mukoba amekamatwa katika ukumbi wa Chimwaga mjini Dodoma ambako kunafanyika uchaguzi wa kujaza nafasi zilizo wazi ikiwemo ya rais, aliyoiacha wazi baada ya kustaafu.


Nafasi nyingine ni katibu mkuu iliyoachwa wazi baada ya aliyekuwa akiishikilia Yahaya Msulwa kufariki dunia.


Mkutano wa CWT ulianza juzi na ulifunguliwa na Rais John Magufuli aliyeonya kuhusu matumizi ya fedha katika uchaguzi.


Rais Magufuli aliwataarifu walimu kuwa Takukuru ipo na inafuatilia uchaguzi huo.


Katika mkutano huo, Rais Magufuli alisema kuna mmoja wao aliwakimbia Takukuru mkoani Singida walipofuatilia tuhuma za ugawaji wa rushwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527