WAUAWA KATIKA VURUGU ZA KUIBIANA BANGI HUKO TARIME

MAPAMBANO ya kutumia silaha za jadi yakiwemo mapanga kati ya wakazi wa Kijiji cha Wegita na Nkerege wakituhumiana kuibiana bangi mashambani, yamesababisha vifo vya watu wawili na wengine wawili kujeruhiwa.

Waliouawa ni Magoro Isaro(35) na Kisyeri Isaro(20) wa kijiji cha Wegita . Ugomvi kati ya familia ya Mwita Mgaya Kinusu wa kijiji cha Wegita na familia ya Makanga Kihugi wa Kijiji cha Nkerege baada ya kutuhumiana kuibiana bangi katika mashamba ya familia ya Makanga, ulithibitishwa na kamanda wa Polisi Tarime/Rorya.

Kamanda wa Polisi Tarime Rorya, Henry Mwaibambe amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kudai familia ya Makanga ilidai kuibiwa bangi shambani ekari tatu iliyovunwa usiku na watu wasiojulikana na kuanzisha vurugu kubwa iliyosababisha vifo. 

Aidha ugomvi ulianza, baada ya familia ya Makanga kuhusisha familia ya Mwita na kuanza kuwashambulia watu waliokuwa wakitoka kijiji cha Wegita kwa mapanga, mishale na mikuki na kusababisha vifo vya wakazi wa wawili wa kijiji jirani cha Wegita.

“Katika vurugu hizo mbali na kuuawa watu hao wawili Magoro na Kisyeri, katika familia ya Makanga watu wake wawili pia nao walijeruhiwa ambao ni Matinde Makange(44) na Nyakirugi Mirumbe ambao kwa sasa wamelazwa katika kituo cha afya Wegita wakiwa chini ya ulinzi wa Polisi huku tukiendelea kuwasaka wote waliohusika katika mauaji hayo,” alisema.

Kamanda Mwaibambe alitoa mwito kwa wakazi wa vijiji hivyo kuacha kujichukulia sheria mkononi na kwamba inaendesha kufanya msako wa watu wanaolima mashamba, kuuza na kuvuta banki na kwamba msako huo utakuwa endelevu katika vijiji vya Wegita, Nyarwana, Nkerege na Kemange vinavyosifika kwa kilimo hicho haramu.

Mwaka huu tayari zaidi ya ekari 50 zimeteketezwa na kamati ya ulinzi na usalama katika vijiji hivyo ambapo Kamanda Mwaibambe aliwaonya wakulima hao kuwa hatua za kisheria na msako wa kuwabaini wakulima hao unaendelea na kuwataka wananchi kuacha kujihusisha na kilimo hicho haramu na dala yake walime mazo ya chakula.
IMEANDIKWA NA SAMSON CHACHA- HABARILEO TARIME

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527