RAILA ODINGA KUJITANGAZA RAIS WA KENYA KAMA UHURU KENYATTA ATAAPISHWA

Muungano wa upinzani wa National Super Alliance (NASA) unakusudia kutamtangaza Raila Odinga, kuwa Rais wa Kenya iwapo Rais Uhuru Kenyatta ataapishwa.

NASA umetoa changamoto kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), isithubutu kumtangaza Rais Kenyatta mshindi wa uchaguzi wa urais wa marudio uliofanyika Oktoba 26, ambao Odinga alisusia kushiriki.

Dhamira hiyo ya NASA ilitangazwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Seneta wa Siaya, James Orengo katika mkutano wa hadhara iliofanyika huko Machokos.

Seneta Orengo alisema viongozi wa NASA wameapa kutumia matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8, kumtangaza Odinga kuwa Rais wa Kenya.

“Tutatumia matokeo ya Agosti 8 kumuapisha mgombea urais wa NASA, Raila Odinga kuwa rais iwapo Uhuru Kenyatta atajaribu kutumia matokeo ya uchaguzi wa urais wa Oktoba 26 kuapishwa,” alionya Orengo.

Alisema kwa mujibu wa Katiba, Wakenya wana mamlaka huru na sauti zao lazima zisikilizwe.

“Mamlaka ya utendaji ya Jamhuri ya Kenya iko mikononi mwa watu wa Kenya, Katiba inasema mna mamlaka huru. Kenyatta hana mamlaka huru bali watu mnayo,” alisema Seneta Orengo.

Aidha, aliwakumbusha jinsi Odinga alivyopambana kuhakikisha Kenya inapata demokrasia kwa kueleza kuwa Odinga alipambana na Kenyatta wa kwanza mpaka akafariki na kwamba aliyekuwa rais wa Kenya Daniel Arap Moi alienda nyumbani baada ya kumfunga Odinga.

Alisema Kibaki alitaniana na Odinga akaenda nyumbani hivyo Kenyatta atakwenda nyumbani na Odinga atakuwa Rais wa Kenya.

Odinga awataka Uhuru, Ruto wakome kumuita mzee
 Jana Kiongozi huyo wa National Super Alliance (NASA), Odinga, aliwataka Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto wakome kusema ni mzee anayepaswa kustaafu siasa na kwamba hastaafu kwa shinikizo.

Akizungumza katika mkutano wa Kitongoji cha Kawangware, Nairobi, Odinga alisema atajiuzulu baada ya kuwakomboa Wakenya kutoka kwenye serikali aliyoiita ya kifisadi ya Jubilee au moyo wake utakapotaka.

“Nitasfaafu siasa si kwa sababu Uhuru na Ruto wameniambia cha kufanya bali nitakapofanikiwa kuwaunganisha Wakenya na kuwafikisha katika nchi ya ahadi.

“Hutakiwi kujikita katika umri wa mtu bali ubongo wake na ajenda na mawazo yake. Kuna vijana wadogo wenye uwezo mdogo wa kuongoza watu,” alisema Odinga.

Odonga alikwenda mbali zaidi kwa kuwaita wapumbavu na wanaopaswa kupuuzwa wanaohoji kuhusu umri wake.

Alikishambulia Jubilee kuwa kinafanya kila linalowezekana kung’ang’ania madaraka ili kuendeleza ukabila na kuwatesa Wakenya kwa gharama kubwa za maisha ya watu.

Odinga ambaye alijitoa katika uchaguzi wa marudio wa urais wa Oktoba 26, alisema NASA ni chama pekee cha siasa chenye suluhu ya matatizo yanayowakabili Wakenya.

“Chini ya Jubilee hakuna kitakachobadilika, mateso yale yale yataendelea. NASA itatengeneza fursa za ajira kwa vijana, mfuko maalumu wa kuwasaidia kina mama wanaolisha familia zao na kukomesha ukabila nchini Kenya,” alisema Odinga.

Awali akiwa kanisani katika kitongoji hicho hicho, Odinga alilaani machafuko yaliyoibuka eneo hilo na kusababisha vifo vya watu watatu Ijumaa iliyopita.

Katika tukio hilo, makundi mawili pinzani yalipambana katika eneo hilo huku taarifa kutoka kwa wenyeji wa eneo hilo zikieleza kuwa kundi lililoharamishwa la Mungiki lilitumwa na wanasiasa kuwasumbua wakazi wa Kawangware wanaohesabiwa kuwa ngome ya upinzani.

Mkakati wa kumng’oa Uhuru
Juzi Odinga alisema vuguvugu la Taifa la Ukombozi (NRM), litahakikisha Uhuru anang’oka madarakani iwapo atatangazwa mshindi na IEBC.

Alisema NRM haitatumia machafuko kuing’oa madarakani Serikali ya Jubilee bali harakati za amani

Kiongozi huyo wa upinzani, ambaye jana aliwashutumu polisi kwa kuua waandamanaji mjini Nairobi pia alisema hawatatumia mandamano kama Jubilee wanavyodai.

Hata hivyo, hakufafanua njia ambayo NRM itatumia kuhakikisha mpango huo kabambe unafanikiwa.

“Hatutatumia machafuko kupambana na serikali. Tutatumia vuguvugu la upinzani kwa amani, si kupitia maandamano bali njia nyingine,” Raila alisema wakati akihojiwa na Shirika la Habari la Marekani (CNN).

Alisema vuguvugu lao litatoa maelezo ya hatua watakazochukua leo kuilazimisha serikali ikae pembeni.

“Jumatatu (leo), tutatangaza mlolongo wa hatua tutakazochukua ili kuibana serikali ing’oke,” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post