KAULI YA MKUU WA MKOA WA DODOMA BAADA YA KUTUMBULIWA NA RAIS MAGUFULI

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wa zamani, Jordan Rugimbana amesema hakuna kilichobadilika kwake kwa sababu mtumishi wa umma ni kama askari ambaye hachagui uwanja wa kupigana vita.


Rugimbana aliyeachwa katika mabadiliko madogo ya wakuu wa mikoa yaliyofanywa na Rais John Magufuli amesema hayo leo Jumatatu Oktoba 30, 2017 alipokabidhi ofisi kwa mkuu mpya wa mkoa huo, Dk Binilith Mahenge.


Akizungumza kuhusu mabadiliko hayo, Rugimbana amesema, "Mtumishi wa umma ni kama askari, hachagii uwanja wa kupigana vita, kwa lugha nyingine hakuna kilichobadilika nipeni muda mtaelewa."


Amesema anakwenda uraiani lakini jukumu lake sasa litakuwa ni kulipa fadhila kwa Rais Magufuli kwa kumchagua kuwa miongoni mwa wasaidizi wake wa kwanza katika Serikali aliyoiunda mwaka 2015.


Rugimbana amesema anachomuahidi Rais ni kuwa atakuwa raia mtiifu, mwaminifu na ataendelea kuwa timu Magufuli.


Amewasifu wakuu wa wilaya akisema ni watiifu, wamekuwa wakiuliza na kupokea ushauri wanaopewa.


Kuhusu utendaji wake, Rugimbana amesema mchakato wa Serikali kuhamia Dodoma unakwenda vizuri.


Mrithi wake, Dk Mahenge amesema atasimamia na kufuatilia mambo yote yaliyofanywa na Rugimbana kwa sababu ni maelekezo ya timu aliyokuwa akifanya kazi nayo.


"Nitasimamia na kufuatilia yote uliyoyafanya kwa sababu ni maelekezo ya timu yako. Wewe ni hazina uendelee kutushauri," amesema

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527