CCM SINGIDA : NYALANDU KAHAMA CCM KWA HASIRA ZA KUKOSA UWAZIRI


Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida kimesema sababu zilizotolewa na aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu za kuacha ubunge hazina mashiko, isipokuwa kilichomsukuma kufikia uamuzi huo ni hasira za kukosa uwaziri.

Katibu wa CCM mkoani Singida, Jamson Mhagama alisema jana Jumatatu Oktoba 30,2017 kuwa, “Kwa maono yake ameona siasa za nchi haziendi vizuri na kuamua kwenda kusaka siasa zitakazompendeza, tunamtakia kila la kheri. Ila tunamwonya kuwa asitarajie tena kupata ubunge kupitia Chadema anakolilia kwenda, CCM itashinda kwa kishindo katika uchaguzi mdogo ujao,” alisema.

“Wananchi walimwamini Nyalandu katika vipindi vyote vinne kwa kumpa kura za kutosha za nafasi ya ubunge. Kupitia kura hizo, Nyalandu amesifika na kujulikana kila kona sasa ameamua kuwapa kisogo wakazi wa jimbo la Singida Kaskazini, jina lake linaenda kufutika na hatasikika tena,” amesema Mhagama.

Katika hilo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Singida, William Mwang’imba amesema kwa jumla wilaya haina shida na Nyalandu na kwa kuwa ameamua kuondoka, basi aende salama.

Tofauti na kauli hizo za CCM, Chadema Mkoa wa Singida imempongeza Nyalandu kwa uamuzi wake, ikisema milango ipo wazi kwa yeye kujiunga na chama hicho.

Mwenyekiti wa Chadema mkoani Singida, Shaban Limu amesema kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, wanapokea mtu yeyote kutoka kokote kuwa mwanachama.

“Alichofanya Nyalandu ni sahihi. Wapo baadhi ya viongozi wakiwemo mawaziri na wabunge hawaridhishwi na hali iliyopo sasa lakini ni waoga, wanaogopa kupoteza masilahi yao,” amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527