SERA ZA KUMWEZESHA MWANAMKE HAZIENDANI NA MAZINGIRA YA KUELEKEA TANZANIA YA VIWANDA NA UCHUMI WA KATI



Imeeelezwa kuwa sera mbalimbali za kumwezesha mwanamke na kuinua usawa wa kijinsia nchini haziendani na mazingira ya sasa katika kuelekea Tanzania yenye viwanda na uchumi wa kati.

Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Mtandao,Vicensia Shule(pichani) wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu masuala mbalimbali yaliyojiri wakati wa siku nne za Tamasha la Jinsia mwaka 2017 lililofanyika katika viwanja vya TGNP Mtandao jijini Dar es salaam kuanzia Septemba 5 hadi 8,2017.

Alisema miongoni mwa masuala yaliyoibuliwa na washiriki wa Tamasha hilo katika siku hizo nne ni pamoja na sera za kumwezesha mwanamke kutoendana na mazingira ya sasa mfano mitaala ya elimu iliyopo haiendani na sera ya kuelekea Tanzania yenye viwanda na uchumi wa kati.

Alisema washiriki wa tamasha hilo wamependekeza sera zifanyiwe marejeo ili ziendane na muktadha wa sasa na ziwe na mrengo wa kijinsia.

“Sera hizo pia ziendane na miongozo na mikakati mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kama vile malengo ya maendeleo endelevu,ajenda ya Afrika 2063,Mkataba wa Jinsia na Maendeleo wa SADC,Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano na mpango wa taifa wa kutokomeza ukatili wa kijinsia”,alieleza Shule.

Katika hatua nyingine alisema ni vyema sasa bajeti kuu za serikali za mitaa zikazingatia mahitaji ya kijinsia kwa makundi yote huku akisisitiza kuwa ziwe za kutekelezeka na mchakato wa kuandaa bajeti uwe shirikishi na wa uwazi bila kujali tofauti za kijiografia,rika,hali ya uchumi,jinsi,elimu na hali ya ulemavu.

“Utengwaji wa rasilimali pia bado ni changamoto hasa katika kukuza na kuendeleza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake,mfano ni asilimia 20 ya wanawake Tanzania wanamiliki ardhi”,aliongeza Shule.

Tamasha la Jinsia la 14 mwaka 2017 lililokutanisha washiriki zaidi ya 1500 kutoka ndani na nje ya Tanzania, limehitishwa leo Septemba 8,2017 baada ya siku nne za sherehe,tafakuri,mijadala na pongezi.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Mtandao,Vicensia Shule akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Ijumaa Septemba 8,2017 katika ukumbi wa TGNP Mtandao
Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Mtandao,Vicensia Shule akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari
Mkurugenzi Mtendaji TGNP Mtandao,Lilian Liundi akizungumza ambapo alisema wataendelea kushirikiana serikali pamoja na mashirika mbalimbali yanayojihusisha na masuala ya kijinsia ili kuhakikisha kunakuwepo na mageuzi ya mifumo kandamizi kwa usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu.
Waandishi wa habari wakiwa ukumbini.

Picha na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post