MADIWANI WALIOANDAMANA NA KUPASUA BOMBA GEITA WATIWA MBARONI,YUMO PIA KATIBU WA UVCCM


Baadhi ya askari pamoja na wafanyakazi wa mgodi huo wakiwa kwenye bomba ambalo limepasuliwa na madiwani wa Halmashauri ya Geita kwa maelezo ya wananchi ambao waliwaona wakifanya uharibifu huo.
Sehemu ya Bomba iliyoharibiwa ikitiririsha maji kwa kasi kubwa zaidi kutokana na tukio ambalo limetokea siku ya jana kwa madiwani kuandamana wakishinikiza mgodi kuwalipa kiasi cha dola Milioni 12.65 ambazo ni deni la mwaka 2004 hadi 2013.
Meneja Mwandamizi wa Masuala ya Jamii Mgodi wa GGM Manase Ndoloma akiwa sehemu ya eneo ambalo lilifanyiwa uharibifu wa kupasuliwa kwa bomba ambalo ndiyo linapeleka maji kwenye chanzo cha maji mgodini hapo.
Shughuli za ukarabati wa Bomba hilo zikiendelea.
Mafundi wakiendelea na shughuli za ukarabati wa Bomba hilo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Geita Mponjoli Mwabulambo akielezea mbele ya waandishi wa habari juu ya hatua ambayo amechukua kwa kuwakamata madiwani sita pamoja na katibu wa UVCCM kutokana na kufanya maandamano ambayo yalikuwa ni kinyume na sheria za nchi. PICHA NA JOEL MADUKA
***

Madiwani 6 wanashikiliwa na Polisi mkoani Geita baada ya kufanya maandamano kinyume cha sheria na kusababisha uharibifu wa Bomba la Maji la kutoka Nungwe kwenda kwenye Mgodi wa Dhahabu wa GGM.

Kamanda wa Polisi mkoani Geita Mponjoli Mwabulambo amesema walichofanya madiwani hao jana hakikubaliki kisheria na kwamba hawakufuata utaratibu wa kufanya maandaman yao na kwamba wanaendelea na msako wa kuwabaini wale wote ambao wamefanya kitendo cha kuandamana na kusababisha baadhi ya kazi kusimama.

Amesema miongoni mwa wanaoshikiliwa ni pamoja na Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM UVCCM wilaya ya Geita kwa tuhuma za kushiriki maandamano na kufanya uharibifu huo.

“Kwa mtu wa kawaida sidhani kama alipendezwa na kitendo hicho tuache habari ya kuremba na kupepesa macho lile tukio sidhani kama ni kitendo kizuri, ni kosa ambalo walilitenda na kwamba tunawashikilia madiwani sita akiwemo katibu wa umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Geita na hicho hakikuwa kizuri lakini pia kukimbia kwao niseme sio suluhisho tutawakamata”,alisema Mponjoli.

Meneja Mwandamizi wa Mahusiano ya Jamii kwenye mgodi wa GGM Manase Ndoloma amesema taarifa za kupasuliwa kwa bomba hilo linalotoa maji safi kutoka ziwa Victoria kupitia kwenye kijiji cha Nungwe hadi kituo cha usambazaji maji kwenye Bwawa la Nyakanga walizipata kwa wananchi na ameahidi kuendelea kushirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo kwenye maeneo yao na kwamba mgodi haujaathirika kwa kutobolewa kwa bomba hilo.

“Tungependa kufanya shughuli zetu za kutekeleza miradi ya kuisaidia jamii ya Geita kwa hali ya usalama lakini pia kwa usalama wa wafanyakazi wetu mgodi wa dhahabu wa Geita utaendelea kushirikiana kwa ukaribu na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na jamii inayozunguka eneo la mgodi ili kuharakisha urejeshaji wa maji pamoja na amani kwa ujumla ndani ya mji wa Geita,alisema Manase.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Nungwe Revocatus Masatu amesema aliwaona watu kutoka halmashauri na magari ya serikali na hakuwa na taarifa yoyote kuhusu kupasuliwa kwa bomba hilo kwani alijua ni taratibu kwa halmashauri kutembelea vijiji vyake.

IMEANDALIWA NA MADUKA ONLINE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527