KAULI YA WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA KUHUSU WATU WASIOJULIKANA


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali haitafumbia macho matukio ya mashambulizi wanayofanyiwa watu mbalimbali wakiwepo viongozi na kuwataka wabunge na wananchi kuendelea kuwa wavumilivu wakati jeshi la polisi likiendelea kufanya uchunguzi.


Waziri Majaliwa amesema hayo wakati akiahirisha vikao vya mkutano wa nane wa bunge la 11, na kusema vyombo vya dola vinaendelea kufanya uchunguzi ili kuwabaini watu wasiojulikana wanaojihusisha na vitendo hivyo  ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

"Serikali haitofumbia macho matukio ya kihalifu yanayotokea nchini, vyombo vya dola tayari vimeshaagizwa kuhakikisha wanawatafuta wanaohusika na vitendo vya kihalifu na kukamatwa ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao", amesema Waziri Majaliwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama Mhe. Adad Rajabu ameliomba bunge kuongeza muda ili kuweza kukamilisha kazi ya kufanya uchunguzi wa matukio ya kujeruhiwa, kuvamiwa pamoja na kufuatiliwa kwa baadhi ya wabunge ili kuweza kukamilisha kazi hiyo.

Aidha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amehairisha vikao vya bunge leo hadi  Novemba 7 mwaka huu ambapo litafunguliwa tena.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527