ASILIMIA 82 YA WASICHANA HAWANA TAARIFA SAHIHI KUHUSU HEDHI


Afisa Sera kutoka TAWASANET,Darius Mhawi katika warsha ya Afya na Maji wakati wa Tamasha la Jinsia mwaka 2017 linalofanyika jijini Dar es salaam

*****
Imeelezwa kuwa asilimia 82 ya wasichana nchini Tanzania hawana taarifa sahihi kuhusiana na mabadiliko ya miili yao na namna sahihi ya kukabiliana na changamoto kipindi cha hedhi hali inayosababisha baadhi yao kushindwa kuhudhuria masomo yao shuleni. 

Hayo yamesemwa leo Jumatano Septemba 6,2017 na Afisa Sera kutoka Taasisi ya Tanzania Water and Sanitation Network (TAWASANET),Darius Mhawi katika warsha ya Afya na Maji wakati wa Tamasha la Jinsia mwaka 2017 linalofanyika kwenye Viwanja vya TGNP Mabibo Jijini Dar es salaam. 

Mhawi alisema wasichana wengi hawana elimu kuhusu mabadiliko ya miili yao hali inayosababisha washindwe kuwa katika mazingira safi na salama wanapokuwa katika kipindi cha hedhi. 

Alisema kwa Mujibu wa utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu,Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mwaka 2014/2015 takwimu zinaonesha kuwa msichana mmoja kati ya 10 hushindwa kuhudhuria shule kwa wastani wa siku nne kila baada ya wiki nne hali inayosababisha kukosa masomo shuleni. 

“Hedhi huathiri Wasichana wanapokuwa shuleni kwa kuwafanya kuwa na hofu ama aibu ya kuchafuka,wengine hupata maumivu ya tumbo na kichwa na baadhi kuwa na hisia za kunyanyaswa na wenzao hasa wavulana”,alieleza Mhawi. 

Mhawi alisema ili kuondoa changamoto za hedhi katika ngazi ya shule ni wakati mzuri sasa elimu ya hedhi iingizwe katika mtaala wa elimu,jamii kuvunja ukimya na kutoona aibu kuzungumzia masuala ya hedhi kwa rika zote katika jamii. 

“Inatakiwa pia kuwepo na upatikanaji wa vifaa salama kwa ajili ya udhibiti wa hedhi na kwa gharama nafuu,kuwepo kwa vyoo bora katika mazingira ya shuleni na utoaji wa huduma ya maji safi na sabuni”,aliongeza Mhawi. 

Nao washiriki wa warsha hiyo waliziomba halmashauri za wilaya kutenga bajeti maalum kwa ajili ya kushughulikia changamoto za hedhi kwa wasichana shuleni. 

Kwa upande wake Rehema Zobonko kutoka halmashauri ya Kisarawe mkoa wa Pwani alizishauri halmashauri za wilaya nchini kuwa na bajeti zinazozingatia masuala ya kijinsia na kutoa taulo laini bure kwa wasichana na kutenga vyumba maalum kwa ajili ya watoto wa kike kujihifadhi wanapokuwa katika hedhi. 

Na Kadama Malunde-Malunde1 blog - Dar es salaam 
Afisa Sera kutoka TAWASANET,Darius Mhawi akizungumza katika warsha ya Afya na Maji wakati wa Tamasha la Jinsia mwaka 2017 linalofanyika jijini Dar es salaam.
Washiriki wa warsha hiyo wakifuatilia mada ukumbini.
Diwani wa kata ya Songwa halmashauri ya Kishapu mkoani Shinyanga Mohammed Ngolomole akichangia hoja katika warsha ya maji na afya
Washiriki wakiwa ukumbini.
Afisa Sera kutoka TAWASANET,Darius Mhawi akisisitiza jambo wakati wa warsha hiyo.
Washiriki wa warsha hiyo wakiwa katika kazi ya kikundi. 
Washiriki wa warsha hiyo wakijadiliana.
Rehema Zobonko kutoka halmashauri ya Kisarawe mkoa wa Pwani akiwasilisha kazi ya kundi lake.
Picha na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post