Mtuhumiwa wa mauaji ya watoto wawili, Moureen David (6) na Ikram Salum (3), amekiri kuwateka watoto hao, kuwaua na kuwatumbukiza ndani ya shimo la maji taka.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, mtuhumiwa Samson Peter (18), alipomaliza kuwateka watoto hao na wengine kuwaachia, alikimbilia mkoani Geita ambako alikamatwa Septemba 2 mwaka huu kisha kuletwa jijini Arusha, Septemba 4, mwaka huu.
Kamanda Mkumbo alisema baada ya mahojiano, Peter alikiri kuwateka watoto hao na wengine kuwaachia kisha kukiri kuwaua Ikram na Moureen na kuwatumbukiza ndani ya shimo la maji taka lililopo katika nyumba ambayo haishi mtu na haijamalizwa kujengwa iliyopo eneo la Mtaa wa Olkerian katika Kata ya Olasiti. Alisema askari baada ya kufika eneo hilo huku wakiwa na mtuhumiwa huyo, waliikuta miili ya watoto hao ikiwa inaelea juu ya maji yaliyopo ndani ya shimo hilo.
Aliongeza kuwa licha ya matukio hayo mawili, mtuhumiwa huyo Agosti 28, mwaka huu saa 11:45 jioni eneo la Kwamrombo, aliwateka watoto wawili ambao ni Ayub Fredy mwenye umri wa miaka mitatu na miezi minne na Bakari Suleiman mwenye umri wa miaka mitatu na miezi miwili na baada ya juhudi za Jeshi la Polisi na wananchi, walifanikiwa kuwapata watoto hao siku hiyo hiyo muda wa saa 2:00 usiku.
Alisema polisi kwa sasa wanaendelea kumhoji mtuhumiwa huyo ambaye anatarajia kufikishwa mahakamani muda wowote mara upelelezi utakapokamilika.
Awali, Mwenyekiti wa Mtaa wa Olkerian, Daudi Safari alisema wazazi wa watoto hao wanasubiri uchunguzi wa kitaalamu wa madaktari ili waruhusiwe kuchukua miili hiyo na kwenda kuizika kwani imeharibika vibaya na kusisitiza kuwa mtoto Ikram atazikwa muda wowote leo baada ya kukamilika kwa taratibu hizo za kiuchunguzi.