WAZIRI MKUU AKATAA OMBI LA WABUNGE WA TABORA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekataa ombi la wabunge wa Ulyankulu na Kaliua ya mkoani Tabora ya kuigawa Wilaya ya Kaliua ili kusogeza huduma kwa wananchi waishio kwenye kata na tarafa zilizo mbali.


Hii si mara ya kwanza kwa kiongozi wa juu wa Serikali kutamka hadharani kwamba hawatagawa maeneo mapya utawala.


Julai mwaka jana akiwa katika ziara ya kikazi katika mkoa huo, Rais John Magufuli pia alikataa ombi la kuugawa Mkoa wa Tabora akisema haoni umuhimu wa kufanya hivyo na badala yake fedha hizo zielekezwe katika kuboresha miundombinu ya barabara, maji na huduma za afya.


“Nataka huduma kwanza mkoa baadaye, huwezi ukaigeuza kila wilaya ikiwa mkoa. Kila unapotengeza mkoa Serikali inaingia gharama. Ninataka niseme ukweli ni nafuu tutekeleze ahadi kwanza,” alisema Rais Magufuli katika ziara hiyo.


Awali, Februari mwaka huu, Rais Magufuli aliridhia kuanzishwa kwa wilaya mpya za Songwe, (Mkoa wa Songwe), Kibiti (Pwani), Kigamboni na Ubungo (Dar es Salaam), Malinyi (Morogoro) na Tanganyika (Katavi).


Kabla ya kutangaza wilaya hizo, mwaka 2015, Serikali iligawanya baadhi ya majimbo mbalimbali kutokana na ukubwa na kupata majimbo mapya 26.


Miongoni mwa majimbo hayo ni Kibamba, Kigamboni, Makambako, Butiama, Tarime Mjini, Bunda Mjini, Tunduma, Newala Mjini, Mbagala, Vwawa, Mafinga Mjini, Nanyamba, Handeni Mjini, Ushetu, Nzega Mjini, Ndanda na Madaba.


Jana, akiwa katika mikutano ya hadhara iliyofanyika Ulyankulu na Kaliua ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Tabora, Majaliwa aliwaambia wananchi na wabunge hao kwamba Serikali imesitisha mchakato kutoa maeneo mapya ya utawala hadi itakapotangazwa vinginevyo.


Akijibu maombi ya wabunge hao Magdalena Sakaya (Kaliua) na John Kadutu (Ulyankulu), ambao walisema kuna haja ya kuigawa Wilaya ya Kaliua ili kusogeza huduma kwa wananchi waishio kwenye kata zilizo mbali na tarafa Majaliwa alisema, “Tumesitisha kutoa maeneo mapya ya utawala ili tuimarishe kwanza yale ya awali. Tunaimarisha kwanza miundombinu ya majengo ya ofisi, nyumba za watumishi kwenye wilaya na halmashauri mpya, zikitengamaa tutafanya uamuzi upya.”


Kuhusu migogoro baina ya wanavijiji na maeneo ya hifadhi, Majaliwa alisema Serikali bado inafanya uhakiki wa mipaka katika maeneo ya hifadhi na ikikamilisha mchakato huo na itatoa taarifa.


Ili kuharakisha mchaktato huo, Majaliwa aliwataka wananchi wanaoishi pembezoni mwa vijiji vinavyopakana na maeneo ya hifadhi wasifanye upanuzi wowote hadi uhakiki wa mipaka utakapokamilika.


“Tumeamua kuweka beacons katika maeneo yote ya hifadhi ili kubaini mipaka imepita wapi. Wananchi mkiwaona watu wa hifadhi wanapita huko msigombane nao. Ni hatua ya awali ya kubaini maeneo ya mipaka,” alisema.


Awali Mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena Sakaya alimweleza Majaliwa kwamba wananchi wanashindwa kujenga makazi ya kudumu katika maeneo waliyopo kwa sababu wanatishiwa kwamba wapo hifadhini.


Hata hivyo, Majaliwa alisema Serikali inafanya mapitio na ikilazimu, itabidi ifanye marekebisho ya sheria inayohusu Misitu ya Hifadhi pamoja na sheria inayohusu masula ya wakimbizi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post