TUNDU LISSU AFICHUA KILICHOCHELEWESHA BOMBADIER KUFIKA

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amedai kuwa ndege aina ya Bombardier Q 400-Dash 8 iliyonunuliwa na Serikali, imezuiwa nchini Canada kutokana na Serikali kudaiwa fidia.

Ndege hiyo ilitakiwa iwasili nchini mwezi uliopita, lakini hadi sasa hakuna taarifa kuhusu ujio wake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Lissu aliyekuwa ameongozana na Freeman Mbowe, ambaye ni mwenyekiti wa Chadema na Frederick Sumaye (mwenyekiti wa Kanda ya Pwani), alisema ndege hiyo inashikiliwa na kampuni ya Stirling Civil Engineering Ltd inayoidai Serikali dola 38.7milioni sawa na Sh87bilioni.

Alisema kutokuja kwa ndege hiyo kama ilivyopangwa licha ya kukamilika, kunatokana na maamuzi yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne, wakati huo Rais John Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi, wa kuvunja mkataba wa kampuni hiyo ya Canada iliyokuwa ikijenga barabara ya Tegeta Wazo-Bagamoyo.

Lissu, ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki, alisema baada ya uamuzi huo, Stirling ilifungua kesi Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi, ikidai kukiukwa kwa mkataba na ilipofika Juni 2010, mahakama hiyo ilitoa tuzo ya ushindi kwa kampuni hiyo, ikiitaka Serikali ilipe fidia ya dola 25 milioni za Kimarekani, huku deni hilo likiwekewa riba ya asilimia nane.

Kwa madai ya Lissu, Serikali ilikataa kulipa fidia hiyo hadi Juni 30 mwaka huu wakati mahakama hiyo ilipoipa Stirling kibali cha kukamata mali zote za Tanzania zitakazokuwa katika nchi za Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ubelgiji, Uganda na Canada.

Lissu ameibua tuhuma hizo miezi mitatu baada ya Serikali kutangaza kuwa ndege hiyo mpya ingewasili Julai.

Akizindua safari za Kampuni ya Usafiri wa Anga la Tanzania (ATCL), Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani alisema ndege hiyo aina ya Bombadier Dash 8-Q 400 imenunuliwa kuimarisha huduma za shirika hilo la Serikali.

Alisema hatua hiyo itaiweza ATCL kufikisha ndege nne na hivyo kupanua mtandao wa huduma zake na kufikia masoko ya nchi jirani kama Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Malawi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Lakini kutowasili kwa ndege hiuyo kumeibua maswali na katikati ya wiki, mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe aliandika katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii akihoji mustakabali wa chombo hicho cha usafiri wa anga.

Chini ya swali hiyo, mchangiaji anayeonekana kwa jina la Mbarawa amejibu kuwa kulikuwa na matatizo kidogo yaliyochelewesha na kuahidi kuwa ndege hiyo itawasili mapema.

Akizungumzia suala hilo, Lissu alidai kuwa hata Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Augustine Mahiga alienda Canada kushughulikia suala hilo.

“Waziri Mahiga akatae kama hakuwa Canada Agosti 3 mwaka huu kimyakimya katika mkutano wa maridhiano na kampuni hiyo ili waachie ndege iletwe Tanzania. Wameikamata hadi wapewe dola 12.5milioni,”alisema Lissu.

Alipoulizwa kuhusu madai ya kushikiliwa kwa ndege hiyo, Ngonyani alisema anachofahamu makubaliano ya manunuzi na kampuni inayotengeneza hiyo yamekwamishwa na ratiba za kampuni hiyo yenye zabuni nyingi za kuzalisha ndege.

“Mimi sina taarifa ya kushikiliwa kwa ndege hiyo, ila ninachojua ndege itakuja. Katika makubaliano ilitakiwa ifike Julai, lakini ratiba zao kwa miezi miwili ijayo hadi Oktoba, ndege itakuwa tayari na itakuwa imeshakamilika,” alisema.

“Unajua Bombardier sasa hivi kwenye soko la ndege ndiyo ‘talk of the day (gumzo). Nchi nyingi zinahitaji, kwa hiyo oda ni nyingi na foleni inakuwa kubwa.

“Lissu ni mwanasiasa anayeweza kuzungumza lolote, ila ukweli utajulikana baadaye. Wasipoleta watakuwa wame-breach contract (wamekiuka mkataba) na sidhani kama watafanya hivyo maana wana kazi zetu nyingi.”

Alipoulizwa kuhusu maagizo ya mkataba wake, alisema kwa sasa yuko nje ya ofisi na asingeweza kueleza kwa undani makubaliano ya mkataba huo katika masharti na muda wa matengenezo itakuwaje.

“Hapa sina details zake, nikirudi kutoka safari nitafute,” alisema.

Kuhusu madai ya kampuni hiyo ya Stirling, Ngonyani alisema serikali kudaiwa si jambo la kushangaza. Alisema tangu Serikali ilipoingia madarakani mwaka 2015, wizara hiyo ya ujenzi ilikuwa inadaiwa Sh1.12 trilioni, lakini hadi Julai, tayari limepungua hadi Sh900 bilioni.

“Mimi sina taarifa kuhusu deni hilo ila kikubwa Serikali kudaiwa si big deal (jambo la kushangaza), ila tunafanyaje katika kuyalipa madeni, pengine inawezekana deni hilo likawa ni sehemu ya madeni tunayodaiwa,” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post