MBOWE " KAMA RAIS ATAZUIA WATANZANIA MILIONI 53 KUSEMA,BASI MAWE YATASEMA

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amemtaka Rais John Magufuli kuacha kuwafunga mdomo Watanzania na kuijenga Tanzania kuwa Taifa la hofu.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika mji wa Bomang’ombe jana, kwa takribani dakika 30, Mbowe alisema hata kama Rais atawazuia Watanzania milioni 53 kusema, basi mawe yatasema.

Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni alienda mbali na kusema Chadema imejipanga kuwafungulia kesi wakuu wa wilaya wote waliowaweka ndani viongozi kwa saa 48 katika maeneo yao.

Alisema katika hali ya kutatanisha Rais Magufuli aliyeapa kuilinda Katiba ya nchi amegeuka na kuzuia mikutano ya hadhara ambayo ipo kisheria.

“Siasa katika nchi yetu inaongozwa na Katiba na sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992, lakini katika mazingira ya kutatanisha kabisa Rais amezuia mikutano ya hadhara hadi mwaka 2020,” alisema na kuongeza:

“Rais usiwazuie watu wako kusema, ukiwazuia mawe yatasema. Kama kuna kitu kibaya duniani ni kuvunja Katiba ya nchi, nataka nimwambie huwezi kufunga midomo ya watu milioni 53.”

“Tunajenga nchi ya watu waoga. Rais anataka aonekane ni mbabe, bungeni tunadhibitiwa hadi hotuba zetu lazima zipitiwe na watu wa usalama waseme uondoe hiki. Watu wenye dhambi ndio waoga.”

Mbowe, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Hai alisema hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema mara nyingi kuhusu umuhimu wa viongozi kuheshimu Katiba na akataka iwe mwiko kwa kiongozi kuidharau.

Akizungumzia kamatakamata ya viongozi, alisema hali hiyo ndio inaimarisha zaidi upinzani kuliko wakati wowote ule na kusema watawaburuza kortini wakuu wa wilaya waliokiuka sheria.

Mbowe alisema baadhi ya wakuu wa wilaya wanatumia vibaya sheria ya kuwaweka watu rumande kwa saa 48 akisema wengine wanaitumia kuwakomoa wale wanaotofautiana nao kimtazamo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini alisema hata wale waliokuwa wanashangilia wimbo wa kuisoma namba nao wanaisoma namba hiyo kwa Kiarabu na Kirumi.

“Huu ni wakati wa kupambana zaidi. Wanatutia hofu kwa kutukamata ili tusiseme, lakini nataka kusema saa ya ukombozi ni sasa. Tutaendelea kusema kwa vile ni haki yetu,” alisema,

Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro alisema Chadema ni chama cha siasa na wanapambana na CCM ambayo hawajui kama ni chama kwa vile wakuu wa mikoa na wilaya ndio wamegeuka viongozi wa CCM.

“Yaani wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ndio wamegeuka viongozi wa CCM. Huko nyuma Chadema tukisema tulikuwa tunajibiwa na Kinana (Abdulrahman) au Nape (Nnauye),” alisema.

Kinana ni katibu mkuu wa CCM wakati Nape alikuwa katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho. Kwa sasa ni mbunge wa Mtama.

“CCM iko wapi? Wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa ndio wanabeba ilani ya CCM. Wananchi Hai msiogope. Chadema chini ya Mbowe haitatetereka kamwe,” alisisitiza Meya huyo, ambaye pia amewahi kukamatwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post