MAWAKILI TANZANIA WAMGOMEA RAIS WA TLS TUNDU LISSU


MGOMO wa kutohudhuria mahakamani uliotangazwa na Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Tundu Lissu, umepingwa na kukosa kuungwa mkono baada ya mawakili kujitokeza kwa wingi mahakamani jana huku wakieleza kuwa ni wazo la mtu mmoja na kwamba huenda wanaogoma hawana kesi katika siku hizo mbili.

Katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Arusha, Kagera, Geita na Mara, gazeti hili limeshuhudia mawakili wakiendelea kuwawakilisha wateja wao licha ya agizo la TLS chini ya Lissu, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), kuwaagiza kugoma kwa siku mbili; jana na leo.

Lissu aliwaeleza waandishi wa habari Jumapili kuwa Baraza la Uongozi la TLS limetangaza mgomo wa siku mbili, kupinga uharibifu uliotokana na mlipuko kwenye Ofisi za Kampuni ya Mawakili ya Immma iliyoko Upanga katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Lakini jana, mawakili walikuwapo mahakamani kama walivyoshuhudiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam uwepo wa mawakili wachache ambao ni wakongwe huku idadi kubwa ikiwa ni ya mawakili wapya ambao huenda waliingia kwenye tasnia hiyo hivi karibuni.

Mmoja wa mawakili hao alisema baada ya tukio hilo, kama chama walipaswa kuitwa na kukaa kujadiliana ni jambo gani wafanye na sio wazo la mtu mmoja kwamba wagome. “Haya ni makosa makubwa na ndio maana unaona kuna mgawanyiko kila mtu anaangalia maslahi yake.

Baada ya tukio tungeitwa ili tujadiliane, lakini hali hii inaonesha kuwa hili ni wazo la mtu mmoja na halitekelezeki,” alisema wakili huyo aliyeomba asitajwe jina. Alifafanua kuwa mawakili wengi wamepima uzito wa agizo hilo na kuona kwamba tukio lililotokea si la kuhusishwa moja kwa moja na Polisi kwa kuwa inawezekana kuna tatizo baina ya kampuni na wateja au majambazi wameamua kufanya hivyo.

Wakili mwingine alidai kuwa hawezi kufanya mgomo kwa sababu hauna uhusiano na uanasheria. Alisema wao wanawawakilisha wateja wao hivyo kitendo cha kutofika mahakamani kwa sababu ya mgomo ni kugomea wateja ambao ndio wamewaajiri.

Miongoni mwa mahakimu, aliliambia gazeti hili kuwa shughuli za mahakama zinaendelea kama kawaida na ameona uwepo wa mawakili katika vyumba vya mahakama. Alisema katika kesi zote zilizopo mahakamani hapo ambazo washitakiwa wanawakilishwa na mawakili, walihudhuria, hali ambayo haina utofauti na wakati mwingine.

Baadhi ya mawakili ikiwemo Jeremiah Ntobesya, Nehemiah Nkoko, Alex Mgongolwa ambao licha ya kukataa kuzungumzia mgomo huo, walikuwepo mahakamani kuwawakilisha wateja wao. Kwa upande wa Mahakama Kuu, mawakili walijitokeza kwa wingi kuwawakilisha wateja wao.

Katika Kanda ya Ziwa, mawakili wa kujitegemea wanaofanya kazi katika Mahakama Kuu ya Kanda ya Mwanza na mahakama za wilaya na mkoa kwa mikoa ya Mwanza, Mara na Geita, wameendelea na shughuli zao za kimahakama kama kawaida na hakuna mgomo wowote ulioripotiwa kutokea.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Jaji Robert Makaramba alisema shughuli za mahakama zimeendelea vizuri na hakuna mawakili waliojitokeza kugoma.

Alisema Jaji Mkuu ndiye mtu pekee anayeweza kutoa maamuzi ya mawakili kuja mahakamani au kutohudhuria mahakamani kutokana na kuwa na dhamana ya kisheria ya kuwasimamia mawakili hao.

Alisema kimsingi mgomo huo, hauwezi kuathiri mahakama, isipokuwa kwa sehemu kubwa utawaathiri mawakili wenyewe na wateja wao, ambao aliwatoa hofu wananchi wenye mashauri mahakamani waendelee kupeleka mashauri yao na yatasikilizwa kwa mujibu wa taratibu za mahakamani.

“Maelekezo tunayofuata sisi kama Mahakama juu ya utendaji kazi wetu ni ya Kaimu Jaji Mkuu na siyo ya mawakili,” alisisitiza Jaji Makaramba, na kuonya kuwa hatua iliyochukuliwa na mawakili hao ya kuitisha mgomo, inalenga kuiacha njiapanda mahakama ambayo imepewa jukumu la kuwatumikia wananchi.

Aliitaka TLS kama zilivyo taaluma, zao wana miiko na maadili ya utendaji kazi wao ikiwa ni pamoja na kutoshiriki kwenye mambo ambayo hayatoi huduma kwa wananchi. “Sitaki kuwasemea TLS wana mamlaka na taratibu zao za kufanya kazi, lakini kwa watakaoacha kufika kazini, taratibu zinajulikana mahakamani, tutakuuliza kwa nini hujaja mahakamani,” alifafanua Jaji Makaramba.

Naye Mratibu wa TLS Kanda ya Ziwa, Amri Linusi alisema kutokana na shughuli za kimahakama wapo baadhi ya mawakili waliohudhuria mahakamani na ambao hawakwenda. “Katika hili la mgomo wa mawakili kwenda kutokwenda mahakamani, limekuwa na interpretation (tafsiri) tofauti kwa tukio la kuvamiwa kwa Ofisi ya Kampuni ya Mawakili ya Immma, wengine wanasema ni siasa na wengine wanadai ni maslahi ya watu”, alifafanua.

Kwa upande wake, Wakili Mande Remigius alisema mawakili wameshindwa kugoma kwa sababu maamuzi ya kugoma yamechukuliwa kwa haraka bila kushirikisha Mahakama na Wizara ya Sheria na Katiba nchini.

“Katika mgomo huo watakaoathirika sio mahakama bali ni wananchi ambao hawana hatia yoyote, tuwa kama mawakili tuna wajibu kwa wateja wetu kuwasimamia haki zao, kwa mantinki hiyo ni vigumu kufanya mgomo unamuathiri mteja,” alieleza Remigius.

Gazeti hili lilitembelea Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza na Mahakama ya Biashara na Wilaya ya Nyamagana na kuwakuta baadhi ya mawakili wakiwa kazini huku shughuli za kimahakama zikiendelea kama kawaida.

Mkoani Arusha, mawakili wanachama wa TLS walisema hawawezi kuunga mkono mgomo huo kwa kuwa ni batili na unakiuka maadili ya taaluma hiyo. Wakili Pares Parpay alisema haungi mkono mgomo huo kwa sababu ameingia mikataba na wateja wake ambao ni wananchi na tayari ameshalipwa mamilioni ya fedha kwa kazi hiyo hivyo kugoma ni kumsaliti mteja wake.

Alisema ni aibu kwa mtu kama yeye kuamua kutoka usingizini na kuunga mkono mgomo wa kutokwenda mahakamani kwani mteja wake atashindwa kumwelewa na kauli za namna hiyo zinapaswa kuangaliwa upya kwani zinaweza kutuingiza mahali pabaya bila ya sababu za msingi.

“Sisi kazi yetu ni kuwatetea wateja wetu na kuunga mkono mgomo ni kumwonea mteja wangu aliyenipa pesa nyingi kufanyia kazi mahakamani kwa niaba yake,” alisema na kuitaka TLS kuviacha vyombo vya usalama kufanya kazi yake kikamilifu ili wahusika wachukuliwa hatua kali.

Naye Edmund Ngemela alipinga kuunga mkono mgomo na kueleza kuwa kufanya hivyo ni kuidhalilisha taaluma ya kuwadhalilisha wateja walioingia nao mkataba wa kufanya kazi mahakamani. Alisema mgomo ulipaswa kushirikisha pande zote ikiwemo Mahakama na kama hilo halikufanyika basi mgomo huo ni batili.

Naye Albert Msando alisema ni vigumu kwake kugoma kwani alikuwa na kesi zenye hati ya dharura ya usikilizwaji na kama angegoma zingefutwa na ingekuwa hatari kwake. Msando alisema nchi ni ya amani na kila mmoja anahitaji amani na tukio la mlipuko Immma linalaaniwa na kila wakili, lakini suala la kugoma ni suala binafsi linalopaswa kuangaliwa kwa mapana zaidi na siyo kukurupuka.

Wakili Moses Mahuna alisema haoni sababu ya kugoma kwani kugoma ni kujidanganya kwa kuchukua fedha bila kufanyika kazi, kitu ambacho kinaweza kutafsiriwa kuwa ni utapeli.

Kaimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Deusdedit Kamugisha alisema jana alikuwa na kesi tano katika mahakama hiyo na kesi zote zilikuwa na mawakili wa kujitegemea na wale wa serikali, hivyo hakuona athari yoyote ya mgomo.

Mkoani Mbeya, mawakili mkoani humo wameiuta msimamo wa Lissu kuwa wenye kulenga maslahi yake binafsi na si wanataaluma hiyo. Sambwee Shitambala na Kambu Habibu ni miongoni mwa mawakili ambao wamesema maamuzi ya Lissu, hayana tija kwa mawakili wengine ambapo waliyasema hayo walipotoa maoni yao, walipozungumza na gazeti hili jana katika viunga vya Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.

Wakili Shitambala alisema alichofanya Lissu ni ubinafsi, kwani amelazimika kutoa tamko kutokana na ofisi ya mawakili wanaomtetea yeye kwenye kesi zake imeungua, lakini vitendo vinavyowakuta mawakili kila siku katika utendaji wa kazi zao hajawahi kusema chochote.

Alisema TLS ni chama cha wasomi, hivyo ilipaswa kufuata utaratibu kwa baadhi ya wawakilishi kwenye mikoa kuitwa au kutuma barua ya tamko hilo kiofisi, lakini hakuna kilichofanyika zaidi ya kiongozi huyo kutoa tamko lake binafsi.

Naye Wakili Habibu alisema tayari walikuwa na mashauri mbalimbali mahakamani hivyo kukubali kugoma, kutasababisha mashauri hayo kufutwa na kuongeza kuwa tamko la Tundu Lissu, wamelipata kupitia mitandao ya kijamii hivyo limedhihirisha kuwa na maslahi binafsi na siyo tamko la Chama.

Kwa upande wake, Msajili Msaidizi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, George Helbert alisema mgomo wa mawakili haujaathiri utendaji wa kazi za mahakama kwani kutokuwepo kwa wakili mahakamani kunaweza kuwa na sababu nyingi ikiwemo kuwa na ratiba zingine.

Nacho Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimedai mgomo wa siku mbili uliotangazwa nchini, hauwezi kuwathiri wateja wao kwa hali yoyote ile kwani unalenga kuonesha nafasi ya wanataaluma hao kwa jamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Hellen Kijo- Bisimba alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati chama chake kilipoungana na wanaharakati wa haki za binadamu kwa madai ya kuungana na mawakili wengine, wakipinga kitendo cha kulipuliwa kwa ofisi za Immma usiku wa manane, Jumamosi iliyopita.

LHRC pamoja na Lissu jana walikusanyika katika ofisi za kituo hicho wakiwa wamevalia nguo nyeusi na kufunga vitambaa vyeusi, na kudai kuwa wanaungana na mawakili wengine katika mgomo huo ambao haukufanikiwa.

Bisimba alililaumu Jeshi la Polisi akidai hawana imani nalo katika kuchunguza shauri hilo, madai ambayo yanakinzana na Mkurugenzi Mshirika wa Immma, Sadoki Magai aliyesema wanasheria hao wanaliamini Jeshi la Polisi kwa uchunguzi wake na hawapendi kuweka hisia za tukio lililotokea na chochote.

Imeandikwa na Francisca Emmanuel, Lucy Lyatuu (Dar), Nashon Kennedy (Mwanza), John Mhala (Arusha), Joachim Nyambo (Mbeya). - HABARILEO

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post