MAJAMBAZI YATEKA BASI ASUBUHI NA KUPORA MALI ZA ABIRIA,WAMO MADIWANI



MAJAMBAZI sita wameteka basi la Kampuni ya Safi na likitokea Kijiji cha Mamba wilayani Chunya kwenda jijini Mbeya na kisha kuwapora abiria jana.

Miongoni mwa waliotekwa ni pamoja na baadhi ya madiwani waliokuwa wakielekea mjini Chunya kwa ajili ya kuhudhuria kikao cha Baraza la Madiwani Maalumu kwa ajili ya kupitia na kujadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kilichofanyika jana.

Akizungumzia tukio hilo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Ramadhani Shumbi aliyekuwa mmoja wa waathirika wa uvamizi huo, alisema tukio hilo lilitokea saa moja kasorobo asubuhi katika eneo la Loge.

Shumbi ambaye ni Diwani wa Kata ya Mamba, alisema walipofika eneo hilo lililo na msitu mkubwa, walikuta kuna gogo kubwa lililolazwa na kufunga barabara na kisha walijitokeza watu sita mmoja akiwa amebeba bunduki na wengine mapanga na fimbo.

Alisema watu hao walipiga risasi tatu hewani na kuanza kupiga vioo vya basi wakiwaamuru abiria washuke, lakini iliwachukua abiria takribani dakika 10 wakigoma kushuka kabla ya baadhi walioonekana kutishika zaidi kuanza kushuka kwa kuruka kupitia madirishani.

Alisema baadaye iliwalazimu abiria wote kushuka na ndipo jambazi wakaanza kuwasachi na kunyang’anya fedha taslimu na simu za mikononi huku walioonekana kubisha, wakipigwa.

“Baada ya kushuka tulilazwa chini na kuanza kukaguliwa ambapo walichukua fedha na simu na mimi mwenyewe ni mhathrika wa simu na fedha kidogo nilizokuwa nazo. Ushauri wangu ni kuwa mabasi kama haya yaanze safari saa moja asubuhi badala ya saa kumi na moja ama kumi na mbili,” alieleza diwani huyo.

IMEANDIKWA NA JOACHIM NYAMBO- HABARILEO CHUNYA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527