Mbunge wa jimbo la Tarime vijijini, kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Heche jana alikamatwa na polisi alipokwenda kituo cha polisi cha Tarime kufuatilia kukamatwa kwa Katibu wake.
Mbunge wa Jimbo la Serengeti Marwa Ryoba amesema kuwa polisi walimkamata Heche kutokana na kauli zake ikiwepo kauli ya kutaka kilimo cha bangi kihalalishwe pamoja na kauli yake ya kuzuia shughuli za ACACIA.
"Mhe. Heche alifika Polisi Tarime kwa ajili ya kufuatilia kukamatwa kwa Katibu wake, katika hali ya kushangaza naye akawekwa chini ya ulinzi na RCO na baadae kuelezwa kuwa alikuwa akitafutwa kwa makosa mawili
"Kosa la kwanza ni Kauli aliyoitoa mapema mwaka huu katika mkutano wa hadhara Sirari ya kwamba atapeleka hoja bungeni aiombe serikali ihalalishe kilimo cha bangi na pili kauli yake ya hivi karibuni kuhusu kuzuia shughuli za ACACIA Nyamongo kufuatia Kauli ya Rais kwamba mgodi huo haupo kihalali nchini." alisema Marwa Ryoba
Aidha Mbunge Marwa anasema kuwa Heche alikataa kutoa maelezo yoyote polisi na jeshi la polisi limechukua simu zake zote
"Walimwachia Heche ila wakachukua simu zake zote na kumtaka afike polisi Jumatatu kwa mahojiano. Alikataa kuchukuliwa maelezo yoyote kwa kuwa hakuwa amekwenda Polisi kwa mambo hayo bali kushughulikia kukamatwa kwa Katibu wake, hivyo amejidhamini na kuondoka ila simu zimebaki Polisi" alisema Marwa Ryoba