WAZIRI MKUU AMUAGIZA WAZIRI MWAKYEMBE KULIFANYIA MAPITIO BARAZA LA MICHEZO TANZANIA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe alifanyie mapitio Baraza la Michezo Tanzania (BMT) na iwapo hatoridhika na utendaji wake alivunje.

“Ninamuagiza Waziri mwenye dhamana kufanya mapitio na kutathmnini upya utendaji kazi wa Baraza la Michezo Tanzania juu ya usimamizi wake wa  michezo nchini na kama hataridhika, anayo mamlaka ya kulivunja Baraza hilo.” 

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Julai 5, 2017) katika hotuba yake ya kuahirisha Mkutano wa Saba wa Bunge mjini Dodoma.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano haitafumbia macho usimamizi mbovu na utawala wa michezo usiojali maslahi ya Taifa. “Serikali imeazimia kuimarisha utendaji kwa vyombo vya michezo nchini ili kila mwenye dhamana awajibike ipasavyo.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameipongeza timu ya vijana walio chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys iliyoshiriki na kutoa upinzani mkubwa kwenye mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika.

Amesema licha ya timu hiyo kumaliza ikiwa na jumla ya pointi 4 sawa na timu iliyoshika nafasi ya pili, ila Vijana hao wameonesha vipaji na uzalendo wa hali ya juu kwa nchi yao.

“Msisitizo wangu kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni kuendelea kuwatunza vijana hao, na kusimamia vilabu vya michezo nchini kuwekeza kwenye soka la vijana ili tujenge timu imara kwa miaka michache ijayo.”

Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua umuhimu wa michezo kwa afya, umoja wa kitaifa na kama fursa ya ajira kwa vijana nchini.

“Wiki iliyopita, mkoani Mwanza yamehitimishwa mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA. Wananchi wa Mwanza na Watanzania kwa ujumla wamejionea uwezo wa kimichezo, vipaji na hamasa kubwa iliyopo miongoni mwa vijana wetu kutumia vipaji vyao. “

Amesema Serikali itaendelea kuratibu michezo shuleni, ikiwa ni pamoja na kusimamia  ufundishaji wa michezo kama somo.  “Maelekezo yetu ni kwamba kila Mkoa uwe na shule angalau mbili zenye mchepuo wa michezo na walimu wenye sifa stahiki za kufundisha michezo.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini, wahakikishe kwamba kila shule inakuwa na viwanja vya michezo mbalimbali ili kuwapa fursa wanafunzi kushiriki michezo ili kupandisha na kuinua vipaji vyao.

Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli kwa kuunga mkono jitihada za michezo nchini kwa dhamira yake ya kujenga uwanja mkubwa wa michezo mjini Dodoma kwa kushawishi mataifa rafiki kama vile Morocco ambao wanajenga uwanja huo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post