MKE AMUUA KWA KISU MUME WAKE KWA TAMAA YA KURITHI MALI

Mwanamke mmoja anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumchoma mumewe na kitu chenye ncha kali kinachodhaniwa ni kisu na kumsababisha kupoteza maisha tukio lililotokea Julai 10 mwaka huu majira ya saa 3:00 usiku.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Ahmed Msangi amemtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Jenifer Shedafa (32) mkazi wa Magaka aliyemchoma mumewe Hosea Makoye (45) ambaye ni mfanyakazi wa Shirika la Umeme Tanesco Jijini Mwanza ambapo inasemekana kuwa wawili hao walikuwa na ugomvi wa mara kwa mara ndani ya ndoa yao, hali ambayo iliyopelekea mwanamke kuwa na tamaa ya kutaka kurithi mali.


Inadaiwa kuwa mtuhumiwa alitenda tukio hilo wakati wakiwa wamelala ndipo mwanamke alipoamka na kuanza kumvizia muwewe kisha kumchoma na kitu chenye ncha kali tumboni na kisha kujipanga kwa ajili ya kutoroka eneo la tukio.


Inasemekana kuwa wakati Jenifer anatekeleza tukio hilo majirani walisikia kelele za kuomba msaada hali iliyopelekea kwenda eneo la tukio na kuweza kumkamata mwanamke huyo wakati anataka kutoroka kisha wakatoa taarifa kituo cha polisi na kuweza kushirikiana na wananchi kumkimbiza marehemu Hospitali ya Rufaa ya Bugando lakini baadaye marehemu alifariki kipindi akiendelea kupatiwa matibabu.


Pamoja na hayo, DCP Msangi amesema kuwa polisi wapo katika mahojiano na mtuhumiwa pindi uchunguzi utakapokamilika, mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani.


Kwa upande mwingine, Msangi amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa ajili ya uchunguzi na pindi uchunguzi ukikamilika utakabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post