KATIBU MKUU WA CHADEMA DK. VICENT MASHINJI MATATANI TENA

Katibu Mkuu wa Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vicent Mashinji, amejikuta matatizoni tena, baada ya kuachiwa kwa dhamana mkoani Ruvuma jana.


Muda mfupi baada ya kuachiwa, Dk. Mashinji aliwekwa chini ya ulinzi na kutakiwa kuripoti ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma ili ahojiwe kuhusu kauli yake ya ‘ngedere kulinda shamba’ aliyoitoa kwenye mkutano wa ndani siku chache zilizopita.

Mmoja wa mawakili wanaomtetea kiongozi huyo, Barbabas Pombona, alisema mteja wake alihojiwa kwa dakika 30.


Alisema baada ya viongozi hao kuachiliwa na mahakama kwa dhamana, Dk. Mashinji aliitikia wito wa kwenda kuhojiwa.


“Tuliwaomba polisi japo wamsubiri kwa saa moja hivi ajiandae, ndipo aende kuhojiwa, baadaye tuliitikia wito.


“RPC hatukumkuta, tulielekezwa tumwone RCO (Mkuu Upelelezi wa Mkoa). Tulimwona akamhoji kwa dakika kama 30 kuhusu kauli aliyoitoa ya kulinda shamba dhidi ya ngedere.


Alisema katika mahojiano hayo, Dk. Mashinji alihoji ngedere ni nani.


“Kwa kweli inashangaza mno, maana Katibu Mkuu amewahoji polisi ngedere ni nani, wameshindwa kumjibu,” alisema wakili Pombona.


Alisema baada ya mahojiano hayo, polisi walisema watatoa majibu Agosti 21, kama Dk. Mashinji ana kesi ya kujibu au la.


Dk. Mashinji, anadaiwa kutoa kauli hiyo alipokuwa kwenye kikao cha ndani cha Chadema wilayani Mbinga, Mkoa wa Ruvuma.


Inadaiwa kuwa Dk. Mashinji akiwa katika kikao hicho, alitumia maneno ya kuudhi kwa kuwapa ushauri Watanzania kulinda mazao ya shamba lao ili yasiharibiwe na mnyama aina ya ngedere.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post