JESHI LA POLISI LAWATAKA MAJAMBAZI DAR WAJISALIMISHE NDANI YA SIKU 7

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limetoa siku saba kwa majambazi wote waliowahi kutumikia vifungo na kuachiwa kwa kumaliza vifungo au rufaa, wajisalimishe kwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu.


Kauli hiyo ilitolewa jijini hapa na Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Lucas Mkondya wakati akizungumza na waandishi wa habari. 


Mkondya alisema lengo la kuwaita majambazi hao ni kutaka kupanga utaratibu mzuri ili waone kama baada ya vifungo vyao, wamebadilika na wanajihusisha na shughuli gani kwa sababu walikuwa ni majambazi sugu na walifanya matukio.


“Kuanzia leo (jana) nataka wajisalimishe, wasipojisalimisha wanajua jinsi tunavyowatafuta kwa sababu ni jambazi hatumtafuti kwa kucheka tunamtafuta kwa silaha lengo la kuhakikisha hatusikii milio ya bunduki ikipigwa Dar es Salaam,” alisema Mkondya.


Aidha, Mkondya aliwataka wenyeviti wa serikali za mitaa, kutoa taarifa kama kuna majambazi katika maeneo yao ambao wamechiwa ili polisi wawafuatilie kikamilifu. Katika tukio jingine, jeshi hilo limewakamata watuhumiwa 44 wa wizi wa vifaa vya magari pamoja na vifaa hivyo vya magari.


Alisema watuhumiwa hao walikamatwa kutokana na operesheni maalumu, ambayo inalenga kuwakamata wezi wa vifaa mbalimbali vya magari, ikiwa ni pamoja na wanunuzi wa vifaa hivyo katika sehemu mbalimbali za jiji hili.


Aliongeza kuwa operesheni hiyo iliyoanza Julai 18, mwaka huu na katika operesheni hiyo ambayo endelevu, watuhumiwa hao walikamatwa na baada ya kupekuliwa katika maduka yao walikutwa na vifaa mbalimbali vya magari.


Katika mahojiano na watuhumiwa wote waliokamatwa, wapo walioshindwa kuvitolea maelezo vifaa hivyo ni namna gani na wapi vifaa hivyo wamevipata huku baadhi ya vifaa vikionesha kuwa vimefunguliwa kutoka kwenye magari mengine kwani vimekutwa na namba za magari.


“Watuhumiwa wote bado wanaendelea na mahojiano na uchunguzi bado unaendelea ili kubaini mtandao wote unaojihusisha na wizi huo wa vifaa vya magari ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani kwa hatua zaidi,” alisema Kaimu Kamanda.


Aidha, jeshi hilo linawashukuru wananchi kwa kutoa taarifa na kuwataka wafanyabiashara wa vifaa vya magari kufuata sheria zinazowawezesha kufanya biashara hiyo kihalali. 


Wakati huo huo, jeshi hilo limekamata bastola moja aina ya Browning Patent ikiwa na risasi tisa baada ya majibizano ya risasi kati ya askari polisi na jambazi mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Adam, ambaye alifariki dunia katika majibizano hayo.


Alisema tukio hilo ni la Julai 19, mwaka huu maeneo ya Ubungo Mawasiliano, ambako awali jambazi huyo na wenzake ambao wanaendelea kutafutwa, walishiriki katika tukio la mauaji lililotokea maeneo ya Kinondoni Block 41 ambako mtu mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi.


Baada ya jambazi huyo kuuawa, alipekuliwa na kukutwa na silaha hiyo Browning, na pia alikutwa na sare za kampuni ya ulinzi zisizokuwa na nembo na zenye rangi ya buluu bahari, fulana moja idhaniwayo ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na boti za kijeshi jozi moja, kamba ya mkonge, plasta, bisibisi na maski za mdomo.


Aidha, alisema sare za ulinzi alizokutwa nazo jambazi huyo ndizo zilizoonekana kuvaliwa siku ya tukio la Kinondoni, huku mtuhumiwa aliyekamatwa awali akikutwa na vibao vya namba za magari zenye namba za usajili STK 4704 na T. 503 APG, vocha za Vodacom za Sh 5,000 pisi 10, tabuleti aina Samsung, pasipoti mbili zenye majina ya Salum Malulu na Jeremiah Malulu zenye picha ya mtu mmoja, kitambulisho kinachodhaniwa ni cha Usalama wa Taifa na mihuri minne. 


Alieleza kuwa uchunguzi unaendelea ili kuwapata washiriki wote wa tukio hilo la mauaji ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post