ANUSURIKA KUTAPELIWA MILIONI 5 NA MAAFISA FEKI WA POLISI NA BENKI KUU YA TANZANIA SHINYANGA



Binti anayefahamika kwa jina la Asha Cledo (24) mkazi wa Kata ya Kambarage katika Manispaa ya Shinyanga amenusurika kutapeliwa fedha na matapeli waliojifanya ni maofisa wa polisi na mwingine kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kiasi cha shilingi milioni 5.8 wakati akizipeleka benki ya CRDB mjini Shinyanga.


Tukio hilo limetokea jana Julai 3,2017  majira ya saa nne asubuhi wakati binti huyo akitembea kwa miguu akizipeleka fedha hizo alizopewa na wazazi wake, ndipo akakutana na matapeli hao mmoja akijifanya kuwa ni Ofisa kutoka BOT na mwingine Jeshi la Polisi

Akisimulia tukio hilo binti huyo alisema akiwa barabarani ghafla alizungukwa na matapeli hao wakimueleza kuwa wanataka kumfanyia ukaguzi kwa madai kuna fedha zimepotea kutoka benki kuu na alipokataa ndipo wakaanza kuuvuta mfuko wa pesa alizokuwa amebebea.

Alisema wakati purukushani hizo zikiendelea ndipo wakatokea maofisa wa polisi wakiwa wamevaa kiraia na kumtia nguvuni mmoja wapo huku mwingine akikimbia na hivyo kufanikiwa kumnusuru kuporwa fedha hizo, ambapo mama yake Joyce Egina alizichukua na kuzipeleka benki .

“Nilipokuwa njiani ndipo wakatokea watu wawili na kuanza kuniaimbia kuwa kuna pesa zimepotea kutoka benki kuu hivyo wao wana mashaka na mimi na wanataka kunifanyia uchunguzi na nilipokataa wakadai wao ni maofisa kwa polisi”,alisema Cledo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Jumanne Muliro alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kubainisha kuwa mtuhumiwa ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi wanamshikilia kwa mahojiano na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.

Alisema jeshi la polisi linafanya uchunguzi kuwabaini watu wengine ambao wanahusika na utapeli huo kwa kujifanya wao ni maofisa wa polisi na Benki kuu ya Tanzania ili washughulikiwe.

Muliro alitoa wito kwa wananchi kuwa wanahudhuria mahakamani kutoa ushahidi ambapo mtuhumiwa huyo siyo mara ya kwanza kukamatwa ambapo amekuwa akiachiwa huru kwa sababu ya kukosekana kwa ushahidi.
Na Kadama Malunde- Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post