Picha: SHEREHE SIKU YA FAMILIA WATUMISHI SHIRIKA LA RAFIKI SDO,DC SHINYANGA AKABIDHI HUNDI YA MIL 1 KUNDI LA WAZAWA



Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro (wa pili kutoka kushoto) akikabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni moja kwa wana kikundi cha "Wazawa" Mama Lishe cha mjini Shinyanga, kulia ni mkurugenzi wa Rafiki - SDO, Gerald Ng'ong'a.



MKUU wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro amelipongeza Shirika la Rafiki Social Development Organization – SDO la mkoani Shinyanga kwa kazi kubwa inayofanya ya kuwakomboa mabinti walioko katika makundi maalumu waliokuwa wakiishi katika mazingira hatarishi.


Pongezi hizo zimetolewa Juni 9,2017  katika sherehe za Siku ya Familia kwa watumishi wa Shirika la Rafiki zilizofanyika eneo la Songwa Club wilayani Kishapu mkoani Shinyanga ambapo mkuu huyo alikuwa mgeni rasmi.

Katika sherehe hizo mkuu wa wilaya alikabidhi hundi ya shilingi milioni moja kwa moja ya vikundi vya mabinti waliopo kwenye makundi maalumu kiitwacho “Wazawa” Mama Lishe chenye makazi yake mjini Shinyanga.

Fedha hizo zimetolewa na Shirika la Rafiki kupitia mradi wake wa SAUTI kwa lengo la kusaidia kukuza mtaji wa kikundi hicho baada ya washiriki wake kuamua kuondoka mitaani na kuamua kujishughulisha na shughuli za ujasiriamali wakiendesha mgahawa wa kuuza vyakula.

Akikabidhi hundi hiyo, Matiro aliwataka walengwa wa kikundi hicho kutumia vizuri msaada waliopatiwa na wakawe mabalozi wazuri kwa mabinti wengine ambao bado wako mitaani wakiishi maisha ya dhiki kufanya vitendo visivyofaa ili na wao wabadilike kitabia.

Hata hivyo alisema baadhi ya mabinti walioko mitaani hawafanyi wanayoyafana kwa kupenda kwao bali wanasukumwa hali ngumu ya maisha waliyonayo na kwamba iwapo wataelimishwa na kupewa ushauri mzuri wanaweza kubadilika kama baadhi yao walivyobadilika na kuanza kufanya shughuli za uzalishajimali.

“Nawapongeza wenzetu wa shirika la Rafiki kwa kazi nzuri wanayoifanya, binafsi nimekuwa nikitembelea baadhi ya walengwa na kuona kweli hivi sasa wameamua kubadilika, walisikiliza ushauri wangu, niliwaambia hakuna kisichowezekana iwapo wataamua kuachana na vitendo visivyofaa,”

“Niwaombe sana hakikisheni mnatumia vizuri msaada huu, uwe chachu ya maendeleo yenu, nanyi wenyewe kaweni mabalozi wazuri kwa wengine, waone kumbe wakiamua kubadilika wanaweza kuwa raia wema, na niwaombe ambao bado wanajihusisha na vitendo vichafu waache sasa, wabadilikie, ikishindakana tutawafukuza,” alieleza Matiro.

Matiro alitoa wito kwa asasi za kiraia na wadau wengine wa maendeleo walioko wilayani Shinyanga kufanya kazi zao kama timu kwa kuhakikisha wanagawana maeneo ya kazi badala wote kufanya kazi zinazofanana.

“Mkiendesha shughuli zenu kwa kushirikiana mtaweza kujipanga nani afanye nini na mwingine afanye kitu gani, hii itaondoa nyote kujikita katika uendeshaji wa miradi inayofanana, mkifanya hivyo naamini mtaisaidia serikali yenu katika kuwapatia maendeleo wananchi wake,” alieleza.

Naye meneja mradi wa Rafiki SDO, Mwamini Haruna alisema mradi wa SAUTI pia unashughulika na utoaji wa elimu ya mabadiliko ya tabia kwa mabinti wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 24 ambapo mpaka sasa mabinti 1,560 wamepatiwa simu za viganjani zinazoingiziwa fedha kila miezi mitatu kiasi cha shilingi 70,000.

“Kwa upande huu mradi mpaka sasa una akiba ya vikundi kiasi cha shilingi 132,489,600 na upande wa mikopo kuna shilingi 175,991,600 ambazo walengwa wanakopeshana wenyewe kwa wenyewe, na tayari matokeo chanya yameonekana baada ya wengi wao kuondokana na utegemezi wa wazazi katika masuala madogo madogo,” alieleza.

 Mwenyekiti wa kikundi cha “Wazawa” Mama Lishe, Fatuma Jumanne alimshukuru mkuu wa wilaya kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuwashawishi mabinti waliokuwa mitaani waweze kujikusanya na kuunda vikundi vya uzalishaji mali.

Fatuma alisema baadhi yao waliitikia wito wake ambapo pia walikutana na wawakilishi wa Shirika la Rafiki lililoamua kuwachukua na kuwapatia mafunzo mbalimbali ikiwemo yaliyohusu mabadiliko ya tabia na ujasiriamali na hivi sasa wameamua kuanzisha shughuli za mama lishe.

“Kwa kweli hatuna budi kukushuru sana mkuu wetu wa wilaya kwa juhudi zako ulizozifanya za kutuhamasisha kujiunga kwenye kikundi hiki, tulisikiliza ushauri wako na tumeanza kuona matunda yake, lakini pia tunawashukuru wafadhili wetu shirika la Rafiki,”

“Wao wamewahi kufanya kile ambacho ilikuwa kifanywe na serikali, wametupatia msaada huu, tunaahidi kuutumia vizuri, na tutakuwa mfano mzuri kwa wenzetu wengine ambao bado wako mitaani wakihangaika, na tunaomba msituchoke kila pale tutakapohitaji msaada au ushauri wowote kutoka kwenu,” alieleza Fatuma.



Awali akitoa taarifa ya shughuli zinazotekelezwa na shirika mbele ya mgeni rasmi,Mkurugenzi wa Shirika la Rafiki - SDO, Gerald Ng'ong'a,aliitaja miradi inayotekelezwa na Shirika lake kuwa ni pamoja na mradi wa SAUTI unaolenga kutoa elimu ya mabadiliko ya tabia na afya kwa makundi maalumu na mabinti wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 24 ambao unatekelezwa manispaa ya Shinyanga, kupiga vita mimba na ndoa za utotoni uliopo Kahama mjini.



“Mheshimiwa mgeni rasmi, mradi mwingine ni ule wa kuwaondoa watoto kwenye ajira mbaya katika migodi midogo ya dhahabu iliyopo wilayani Kahama na kata ya Mwakitolyo kwa wilaya ya Shinyanga, ambako mpaka sasa tumefikia watoto wapatao 700 na 411 tayari wamepatiwa mafunzo ya ufundi wa aina mbalimbali,”



“Kwa upande wa mradi wa SAUTI tumefanikiwa kukusanya mabinti kutoka makundi maalumu ambao wameunda vikundi vya uzalishaji mali na tumewapatia mafunzo ya ujasiriamali ikiwemo ya mabadiliko ya tabia na afya, na leo hii tunakipatia kikundi cha Wazawa Mama Lishe msaada wa shilingi milioni moja ili zikuze mtaji wao,” alieleza.

Sherehe hizo pia zilienda sambamba na zoezi la kutoa zawadi na vyeti vya kuthamini kazi kubwa iliyotekelezwa na watumishi wa rafiki - SDO ambapo kwa upande wake mkuu wa wilaya alitunikiwa cheti cha kuthamini mchango anaoutoa kwenye asasi za kiraia katika wilaya yake.


Mwandishi wa Mtetezi wa Haki Blog,Abeid Suleiman ametuletea picha za matukio mbalimbali yaliyojiri wakati wa sherehe za Rafiki SDO Family day..Angalia hapa chini


Mkurugenzi wa Shirika la Rafiki - SDO, Gerald Ng'ong'a akitoa taarifa ya shughuli zinazotekelezwa na shirika mbele ya mgeni rasmi,alisema shirika lake kwa hivi sasa linaendesha miradi mitatu inayotekelezwa katika manispaa ya Shinyanga, halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na Kahama.


Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro akitoa hotuba yake wakati wa sherehe hizo
Wageni waalikwa na Staff wa Rafiki - SDO wakifuatilia kwa makini hotuba ya mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro.
Meneja Miradi wa Shirika la Rafiki - SDO, Mwamini Haruna akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa SAUTI.
Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Rafiki - SDO, Gerald Ng'ong'a akiwa eneo la tukio
Mgeni rasmi, mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro na Mkurugenzi wa Shirika la Rafiki SDO wakifuatilia onesho la wasanii (hawapo pichani) wakati wa sherehe za Siku ya Familia kwa watumishi na wadau wa Shirika la Rafiki.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro (wa pili kutoka kushoto) akikabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni moja kwa wana kikundi cha "Wazawa" Mama Lishe cha mjini Shinyanga, kulia ni mkurugenzi wa Rafiki - SDO, Gerald Ng'ong'a.
Mwenyekiti wa kikundi cha "Wazawa" Mama Lishe, Fatuma Jumanne akifurahia mfano wa hundi mara baada ya kukabidhiwa rasmi na mkuu wa wilaya ya Shinyanga, kulia ni Gerald Ng'ong'a mkurugenzi wa Shirika la Rafiki SDO.
Zoezi la kutunuku hati likaendelea
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine la kutoa zawadi na vyeti vya kuthamini kazi kubwa iliyotekelezwa na watumishi wa rafiki - SDO ambapo kwa upande wake mkuu wa wilaya alitunikiwa cheti cha kuthamini mchango anaoutoa kwenye asasi za kiraia katika wilaya yake.
Mkurugenzi wa Shirika la Rafiki - SDO, Gerald Ng'ong'a akimtunuku mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro, Hati maalumu ya kuthamini na kutambua mchango anaoutoa katika shirika la Rafiki, anayeshuhudia kushoto ni diwani Shella Mshandete aliyekuwa amemwakilisha Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Agnes Machibya. 







Ufunguaji wa Shampeen kwa ajili ya kuashiria kuanza rasmi kwa sherehe ya Rafiki Family Day.

Zoezi la kugonga cheers likiendelea
Cheers!!

Wageni waalikwa na watumishi wa Shirika la Rafiki - SDO wakipongezana kwa kugonganisha grasi za vinywaji vyao na mgeni rasmi (Cheers).
Furaha ikaendelea kutawala eneo la tukio
Sehemu ya wana Kikundi cha "Wazawa" Mama Lishe wakijiandaa kupokea hundi yao.












Burudani ikiendelea

Muziki ukiendelea




Burudani ikiendelea





Picha zote kwa hisani ya Mtetezi wa Haki Blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post