Balaa Jingine Shinyanga: MWANAMKE AJIUA KWA KUJICHINJA KWA KISU NA CHUPA YA SODA




Siku moja tu baada ya mtandao huu kuripoti kuhusu tukio la mwenyekiti wa chama cha waendesha bodaboda manispaa ya Shinyanga Jacob Paul kujiua kwa kujinyonga leo tunayo habari nyingine ya mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Sada Elias (24) mkazi wa mtaa wa Mabambasi kata ya Ndembezi katika manispaa ya Shinyanga ambaye amefariki dunia baada ya kujichinja kwa kisu kisha kupasua chupa ya soda na kujichoma nayo kwenye koromeo.Mwandishi wa Malunde1 blog,Kadama Malunde anaripoti.




Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo wanasema mwanamke huyo aliyekuwa anaishi na mwanae wa miaka mine na mdogo wake aliyejulikana kwa moja la Vesi (12) alichukua uamuzi wa kujiua usiku wa kuamkia Juni 8,2017 majira ya saa nane usiku.

Akielezea kuhusu tukio hilo jirani/mpangaji mwenzake na marehemu,Peter Maduhu alisema siku ya tukio majira ya saa nane usiku,mdogo wake na marehemu aitwaye Vesi alipiga kelele akitoka ndani ya chumba wakichokuwa wanaishi akidai dada yake anajiua kwa kisu.

“Wakati anatoka ndani alikuwa tayari amemunyang’anya kisu, tuliamka kwenda katika chumba hicho lakini mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani,tukaamua kuvunja mlango tukakuta amevunja chupa akijichoma nayo kwenye koromeo,polisi walivyokuja tukampeleka hospitali kwa ajili ya matibabu”,alieleza Maduhu.

Alisema Sada Elias alifariki dunia siku ya Ijumaa majira ya saa tano usiku wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.

Maduhu alisema kabla ya kifo chake,jirani yake huyo ambaye alikuwa anajishughulika na shughuli ya kuuza chakula “Mama Ntilie” alikuwa analalamika kuumwa kwa muda mrefu bila kutaja ugonjwa uliokuwa unamsumbua.

Akisimulia kuhusu tukio hilo baada ya mazishi yaliyofanyika leo Jumapili Juni 11,2017 mchana,Mwenyekiti wa mtaa wa Mabambasi David Nkulila,ambaye pia ni diwani wa kata ya Ndembezi,alisema kifo cha mwanamke huyo kinatokana na msongo wa mawazo.

“Huenda kifo hiki kimetokana na msongo wa mawazo,alikuwa anaishi peke yake na watoto hao wawili,pengine kutokana na ugumu wa maisha na alikuwa analalamika anaumwa,aliamua kujifungia ndani ya chumba chake huku akiwaambia watoto wake kuwa mtu yeyote atakayeuliza kuwa kaenda wapi,wamwambie yupo kazini”,alieleza Nkulila.

Nkulila aliwataka wananchi pindi wanapopata matatizo wasinyamaze kimya bali waombe ushauri kwa watu wanaowazunguka ikiwemo wazee na viongozi wa dini na kuhakikisha wanamshirikisha mwenyezi Mungu.

Naye baba wa marehemu Elias Luleju mkazi wa kata ya Nyakahula wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera aliushukuru uongozi wa mtaa huo kwa ushirikiano waliouonesha wakati wa msiba huo na aliamua kuwachukua watoto aliokuwa anaishi nao marehemu huku akidai mume wa mwanaye yuko wapi.

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro amethitisha kutokea kwa tukio hilo.
Mwili wa marehemu Sada Elias ukiwa umetolewa kwenye msikiti wa Masjid Aqswa Ngokolo A (gari la upande wa kulia) leo majira ya saa saba mchana
Mwili wa marehemu Sada Elias ukishushwa kwenye gari kwa ajili ya mazishi katika makaburi ya Mshikamano Ngokolo mjini Shinyanga
Wananchi wakiwa wamebeba mwili wa marehemu 
Mwenyekiti wa mtaa wa Mabambasi David Nkulila,ambaye pia ni diwani wa kata ya Ndembezi akizungumza baada ya mazishi ya marehemu Sada Elias
Baba wa marehemu Sada mzee Elias Luleju mkazi wa kata ya Nyakahula wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera akiwashukuru wananchi wa mtaa wa Mabambasi kata ya Ndembezi kwa ushirikiano waliompa wakati wa msiba huo kwani yeye anaishi Kagera amefika mtaani hapo kwa ajili ya mazishi na kuchukua watoto waliokuwa wanaishi na marehemu.
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post