Kutoka Ikulu : MKURUGENZI WA EWURA ATUMBULIWA....DUDE LA IPTL LAMPITIA


Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) bwana Felix Ngamlagosi
****

Waziri mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) bwana Felix Ngamlagosi.


Taarifa kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ambayo imesainiwa na Mkurugenzi wake,Gerson Msigwa inaeleza kuwa Ngalamgosi amesimamishwa kazi kuanzia leo Juni 11,2017.

Mwishoni mwa wiki inayomalizika leo Juni 11,2017 Mamlaka hiyo ilitoa taarifa kwa umma kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imepokea maombi ya kuongeza muda wa leseni ya kuzalisha umeme kutoka kwa kampuni ya uzalishaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) (“Mwombaji”). 


EWURA iliuarifu umma na wadau mbalimbali kwa ujumla kuwasilisha maoni au pingamizi ili kufanikisha uchambuzi mzuri wa maombi hayo.

Taarifa za ilitolewa chini ya kifungu cha 19 cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji, Sura ya 414 ya Sheria za Tanzania na kifungu cha 8 cha Sheria ya Umeme, Sura ya 131 ya Sheria za Tanzania.

Tayari wadadisi wa mambo wanahusisha kusimamishwa kazi huko kunatokana na tangazo hilo la kutafuta maoni ya wanachi ya kutaka kumuongezea mkataba IPTL.

Itakumbukwa kuwa Januari Mosi mwaka huu Rais Dk. John Magufuli, alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mhandisi Felchesmi Mramba, katika hali inayoonesha kuwa Rais amekerwa na jaribio la Tanesco kupandisha bei ya umeme.

Baada ya Mramba kutenguliwa nafasi yake alipewa Dk. Tito Esau Mwinuka kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO akimtoa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikokuwa akifundisha.

Rais Magufuli, alichukua hatua hiyo siku mbili baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuiidhinisha ongezeko la asilimia 8.5 ya ya bei ya huduma za umeme kwa kilichoelezwa kuwa lengo ni kukidhi gharama za uzalishaji wa umeme.

Ongezeko hilo lilitangazwa juzi jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, aliyesimamishwa kazi, Felix Ngamlagosi.









Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post