WALIOONEWA SAKATA LA VYETI FEKI WAKATE RUFAA

Serikali, imesema watumishi wa umma walioorodheshwa kwenye orodha ya watumishi wa umma wenye vyeti feki, wakati hawakutakiwa kuwekwa, wakate rufaa.

Kauli hiyo, ilitolewa jana  na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Laurean Ndumbaro, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

“Kama mtakumbuka, uhakiki wa vyeti feki kwa watumishi wa umma, ulihusisha vyeti vya kidato cha nne, kidato cha sita, ualimu na taaluma zingine.

“Baada ya uhakiki huo, iliagizwa watumishi 9,932 waliokuwa na vyeti feki, waondolewe katika ajira, watumishi 1,538 wenye vyeti vyenye utata kwa maana kwamba vinatumiwa na watu zaidi ya mmoja, wathibitishe vyeti vyao kabla ya Mei 15 mwaka huu na mishahara yao isimamishwe hadi uhakiki utakapokamilika.

“Wale watumishi 11,596 waliogundulika kuwa na vyeti pungufu, wanatakiwa kuwasilisha vyeti vyao vikaguliwe kabla ya Mei 15, mwaka huu, vinginevyo watachukuliwa hatua.

“Lakini, wale wanaodai kwamba wamewekwa kwenye orodha ya wenye vyeti feki wakati hawakutakiwa kuwa huko, tunawaomba waandike barua za kukata rufaa kwa Katibu Mkuu Utumishi kupitia kwa waajiri wao.

“Waajiri hao, watatakiwa kuwasilisha vyeti hivyo Baraza la Mitihani la Taifa kwa ajili ya uhakiki zaidi kabla ya Mei 15, mwaka huu.

“Pamoja na hayo, ieleweke kwamba, baadhi ya watumishi wakati wanaajiriwa, waliwasilisha vyeti vya matokeo mengine ya sekondari na wakati wa uhakiki, walionyesha vyeti vingine.

“Lakini, naomba ieleweke kwamba, hakuna mtumishi wa umma mwenye cheti halali atakayeondolewa katika utumishi wa umma.

“Kuhusu suala la mafao ya watumishi hao, hilo tunaliangalia namna ya kulifanya kwa sababu kuna sheria zinazolisimamia,” alisema Dk. Ndumbaro.

Ajira za dharura
Pamoja na hali hiyo, Dk. Ndumbaro aliwataka wakuu wa idara ambazo huduma zake zimeathiriwa na zoezi la vyeti feki baada ya watumishi kuacha kazi kwa kuwataka kuandika barua kwake ili zitangazwe nafasi za ajira za dharura kwa lengo la kuziba mapengo hayo.

Akizungumzia wizara ambazo taarifa za uhakiki wake hazikutolewa hivi karibuni, alisema zitatolewa Mei 10 mwaka huu baada ya uhakiki wake kukamilika.

Katika hatua nyingine, Dk. Ndumbaro alisema Serikali itaajiri watumishi 1,500 kuanzia sasa hadi mwisho wa Bunge la Bajeti linaloendelea mjini hapa.

Kwa mujibu wa Dk. Ndumbaro, ajira hizo zimetolewa ili kukabiliana na uhaba wa watumishi wa umma ulioko katika sekta mbalimbali serikalini.

“Katika hili, waajiri watatakiwa kuhakiki vyeti vya waombaji wote kabla hawajaajiriwa ili kuepuka uwepo wa watumishi wengine wenye vyeti feki,” aliagiza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post