WAZIRI WA AFYA ATAJA VIPIMO NA DAWA ZA MALARIA ZINAZOTAKIWA KUTOLEWA BURE KWA WANANCHI

Serikali ya Tanzania imepiga marufuku vituo vya Umma kuwalipisha wananchi wanaokwenda kupima maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kwa kipimo cha MRDT na utoaji wa dawa za mseto (ALUU) zinazotumika kutibu ugonjwa huo kuanzia sasa.


Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Malaria duniani mjini Dodoma, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Ummy Mwalimu amesema vipimo hivyo ni bure na pia mgonjwa asilipishwe fedha kwa dawa za mseto.


“Napenda kusisitiza vituo vya umma vinavyotumia vipimo vya MRDT kwa wagonjwa wa malaria, vipimo hivyo ni bure na pia mgonjwa asilipishwe fedha kwa dawa za mseto ama yule anayelazwa kuchomwa sindano ya ugonjwa huo….Waganga wakuu wa mikoa na wilaya, hakikisheni kuanzia sasa mnafuatilia wahudumu wote na watakaokiuka agizo hili watachukuliwa hatua za kisheria mara moja”. Alisema Bi. Ummy


Aidha, Bi. Ummy amewataka wananchi kushirikiana na serikali kuwafichua wahudumu wa Afya ambao watawalipisha fedha pindi watakapo kuwa wanapima huduma ya Malaria kupitia kipimo cha MRDT ama watakapohitajika kupewa dawa ya mseto (ALUU), pia amezionya maabara binafsi ambazo zimekuwa zikifanya kazi zake kwa kuangalia zaidi fedha badala ya maisha ya mtu kama kuwaambia wana maambukizi ya malaria wakati hawana.


Pamoja na hayo, amesema takwimu kutoka katika vituo vinavyotolea huduma za afya zinaonyesha takribani watu milioni 12 wanaugua ugonjwa huo kwa mwaka ambapo katika tafiti hizo mkoa wa Kagera, Geita na Kigoma ziliweza kuonekana na viwango vikubwa vya maambukizo kwa mwaka 2015 na 2016 huku wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kuonekana kuathiriwa zaidi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527