Imeelezwa kuwa watu wanaosumbuliwa na ugonjwa wa ini wanaweza kuepuka kifo cha mapema kutokana na ugonjwa huo kwa kusafisha kinywa vizuri hasa kusugua meno na fizi.
Kwa mujibu wa stori iliyochapishwa na Daily Mail April 20, 2017, fizi ambazo hazisafishwi vizuri huzalisha bacteria ambao husafiri hadi kwenye ini na huweza kusababisha kifo kwa mtu anayeugua ugonjwa wa ini ambao unatajwa kuwa ni moja kati ya sababu kubwa za vifo ukikamata nafasi ya tano katika nchi za England na Wales.
Wanasaynsi kutoka Aarhus University Hospital, Denmark, walifanya utafiti kwa watu 184 ambao walikuwa wanaugua ugonjwa wa ini ambapo 44% kati yao walikuwa pia na ugonjwa wa fizi uliosababisha vifo vyao huku mmoja wa watafiti hao Dr Lea Ladegaard Gronkjaer, alisema: “Ugonjwa wa fizi unaweza kuwa chanzo cha kuhifadhi bacteria ambao husababisha uvimbe na matatizo mengine katika ini.”
Ingawa matokeo ya utafiti huo yanashawishi, baadhi ya wataalamu wanaonya kuwa uchunguzi zaidi unahitajika kujua athari na kuimarisha usafi kwa wagonjwa wa ini.
Professor Philip Newsome, Mtaalamu wa Ini, University of Birmingham, alisema: “Utafiti huu umeonesha uhusiano baina ya ugonjwa wa fizi na hatari ya kifo kwa wagonjwa wa ini – tafiti zaidi zinahitajika kujua kama utunzaji wa fizi unaweza kuwa kinga kwa ugonjwa wa ini.”