RAIS MAGUFULI AAGIZA MADAKTARI 258 WALIOTAKA KWENDA KENYA SASA WAAJIRIWE MARA MOJA TANZANIA

Madaktari 258 ambao walikidhi vigezo vya kwenda kufanya kazi nchini Kenya, sasa wataajiriwa na serikali ya Tanzania kutokana na kuwepo na zuio la Mahakama ya Kenya la kuwaajiri.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya Rais Magufuli kumwelekeza jana kuwa awaajiri madaktari hao pamoja na wataalam wengine wa afya 11.

Madakatari hao walioomba hizo nafasi za kwenda Kenya walikuwa 496 kati ya 500 waliotakiwa, 258 ndio wakakidhi vigezo.


Mkataba wa Tanzania na Kenya ilikuwa mpaka Aprili 6 wawe wamepatikana hao madaktari na kati ya Aprili 6 mpaka 10 wasafirishwe kwenda Kenya, sasa baada ya kuajiriwa na serikali, Kenya wakiwa tayari na kuhitaji tena madaktari watatafutiwa wengine.

************

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,
JINSIA, WAZEE NA WATOTO

TAARIFA KWA UMMA 

AJIRA YA MADAKTARI WA TANZANIA NCHINI KENYA

Mnamo tarehe 18 Machi 2017 Ujumbe wa Serikali ya Kenya ukiongozwa na Waziri wa Afya Dkt. Cleopa Mailu uliwasili nchini ambapo ulikutana na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa madhumuni ya kuomba kuajiri kwa Mkataba Madaktari wa Tanzania mia tano (500) ili kupunguza uhaba wa Madaktari nchini Kenya. Mheshimiwa Rais alikubali ombi hilo.


Tarehe 18 Machi, 2017 Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilitangaza nafasi hizo za ajira kwa Madaktari wa Tanzania kwenda kufanya kazi nchini Kenya. Maombi hayo yalipokelewa ambapo hadi tarehe 27 Machi, 2017 ambapo jumla ya maombi takribani 496 yaliwasilishwa. Baada ya kufanya uchambuzi wa maombi haya ilibainika kuwa, Madaktari 258 walikidhi vigezo vilivyotakiwa kwenda kufanya
kazi nchini Kenya. 

Baadhi ya vigezo hivyo ni pamoja na: 

· 
Uhakiki wa vyeti vya taaluma na vyeti vya Sekondari.· 
Chuo alichosoma na mwaka wa kuhitimu masomo.
Sehemu alikofanya mafunzo ya vitendo (Intership) na mwaka wa kuhitimu mafunzo hayo.

Uzoefu wa kazi.

· Umri wa mwombaji usizidi miaka 55.
Usajili wa mwombaji katika Baraza la Madaktari la Tanganyika.
· 
Asiwe mtumishi wa Umma, Hospitali Teule za Halmashauri na Hospitali za Mashirika ya hiyari wanaolipwa mishahara na Serikali.

Wakati Serikali ya Tanzania ikiendelea kukamilisha utaratibu wa ajira za Madaktari wake nchini Kenya ikiwa ni pamoja na kutangaza nafasi hizo za kazi na kufanya uchambuzi wa
maombi ya kazi, kuandaa Hati ya Makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Kenya kuhusu ajira hizo za Madaktari na Mkataba wa Ajira kwa Madaktari hao, wananchi (Madaktari) watano wa Kenya waliwasilisha pingamizi Mahakamani
kuitaka Serikali ya nchi yao kusitisha kuajiri Madaktari kutoka Tanzania. 

Kwa kuwa ratiba ya utekelezaji wa ajira hizi za Madaktari ilikubalika na pande zote mbili kuwa iwe imekamilika ifikapo tarehe 6 Aprili, 2017 na kuwa Madaktari hao wawe tayari kusafiri kwenda nchini Kenya kati ya tarehe 6-10 Aprili, 2017 na kwa kuwa hadi tarehe ya taarifa hii Mahakama nchini Kenya haijaondoa pingamizi lililofunguliwa kuhusu ajira za Madaktari wa Tanzania nchini Kenya, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameamua kuwa,
Madaktari hao 258 ambao waliokuwa tayari kwenda kufanya kazi nchini Kenyawaajiriwe na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara moja.

Kufuatia uamuzi huu, Majina ya Madaktari husika na vituo watakavyopangiwa kazi yatatangazwa katika tovuti ya Wizara www.ehealth.go.tz pamoja na wataalamu
wengine wa Afya 11 walioleta maombi yao na kukidhi vigezo.

Aidha, Serikali ya Tanzania itakuwa tayari kushughulikia upya ombi la Serikali ya Kenya kupatiwa Madaktari 500, pale ambapo hakutakuwa na vikwazo vya kupeleka Madaktari wetu
nchini Kenya. 

Imetolewa na:

UmmyA. Mwalimu (Mb),

Waziriwa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto,

Chuo Kikuu cha DODOMA,S.L.P.743, DODOMA.

Aprili19,2017

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post