MWANAMKE AUAWA KWA KUKATWA MAPANGA SHINYANGA


Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro
***
Mwanamke aliyejulikana kwa jina la Nyanzobe Maganga (50) mkazi wa Kitongoji cha Nzanza kijiji cha Puni kata ya Puni wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga amefariki dunia kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake.Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo wameiambia Malunde1 blog kuwa tukio hilo limetokea jana Aprili 11,2017 majira ya saa tatu na dakika 50 usiku.

Wanasema mwanamke huyo akiwa na mjukuu wake nyumbani kwao sebuleni ghafla walivamiwa na mtu aliyekuwa ameshikilia panga kisha kuanza kuwashambulia ambapo mjukuu alipigwa kwa ubapa wa panga na kuambiwa anyamaze na mwanamke huyo kuanza kukatwa mapanga.

"Mjukuu alipiga kelele kisha majirani walifika kutoa msaada ambapo tayari muuaji huyo alikuwa ameshakimbia...mwanamke huyo alikimbizwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya matibabu lakini alifariki dunia akipatiwa matibabu",wanaeleza mashuhuda wa tukio hilo,

Inaelezwa kuwa huenda chanzo cha mauaji hayo ni mgogoro wa mashamba.

Diwani wa kata ya Puni Heke Kuyela ameiambia Malunde1 blog kuwa mwanamke huyo alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.

Akizungumza kwa njia ya simu na mtandao huu Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa mwanamke huyo alikutwa na majeraha matatu katika mwili wake.

Aidha Kamanda Muliro amesema uchunguzi unaendelea kufanyika juu ya tukio na tayari watu wanne wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi ili kubaini chanzo cha mauaji hayo.

Na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post