MAHAKAMA YAMALIZA MGOGORO WA TIMU YA STAND UNITED FC, KAMPUNI WAPIGWA CHINI


Wachezaji wa timu ya Stand United FC

HATIMAYE Mahakama ya wilaya ya Shinyanga imetoa hukumu yake kuhusiana na kesi iliyokuwa imefunguliwa na kundi moja la wanachama lililojiita Stand United Kampuni likiomba kumilikishwa timu hiyo kutoka mikononi mwa kundi lingine la wanachama wa Stand United.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa na Hakimu mkazi Evodia Kyaruzi, alisema baada ya kupitia maelezo ya pande zote mbili mahakama hiyo imetupilia mbali pingamizi lililofunguliwa na upande wa walalamikaji (Stand kampuni) na kuamua timu hiyo iendelee kumilikiwa na wanachama wenyewe.

Kyaruzi alisema kutokana na hali hiyo timu hiyo itaendelea kuwa chini ya wanachama wenyewe kwa kutumia jina lake lilelile la Stand United Football Club na kubariki rasmi uongozi uliokuwa umechaguliwa na wanachama wenyewe chini ya menyekiti wao, Dkt. Ellyson Maeja na kwamba wanachama ndiyo watakaokuwa na sauti ya mwisho kuhusiana na uendeshwaji wake.

Akizungumza baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mwenyekiti wa timu ya Stand United FC, Dkt. Ellyson Maeja alielezea kufurahishwa na jinsi mahakama ilivyotenda haki ambapo alisema kazi kubwa iliyopo mbele yake hivi sasa ni kurejesha umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama.

Alisema hakuna sababu ya wanachama wa Stand FC kuendeleza mgogoro uliokuwepo na badala yake waungane kuwa kitu kimoja ili kuijenga timu yao kwa kujitolea kwa hali na mali ikiwemo kutafuta wafadhili watakaosaidia ili iendelee kufanya vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom hapa nchini.

“Nimefurahi kwa jinsi mahakama yetu ilivyotenda haki, tunamshukuru mwenyezi mungu kuona suala hili leo (jana) limemalizika, ukweli sisi viongozi tuliochaguliwa na wanachama tulikuwa na wakati mgumu muda mfupi baada ya kuchaguliwa kwetu, tulipambana na changamoto nyingi ikiwemo kuwekewa pingamizi hili mahakamani,”

“Kwa hali hii nawaomba wanachama na wapenzi wote wa Stand United F.C tuungane na kuwa kitu kimoja ili kuiendeleza timu yetu, ambayo kwa sasa ni ya sita katika msimamo wa ligi, tutafute wafadhili wa kutusaidia ili tuijenge kwa ajili ya msimu ujao iwe imara iweze kutwaa taji la ubingwa badala ya timu kubwa za Simba na Yanga zilizozoeleka,” alieleza Maeja.

Maeja aliendelea kueleza kuwa hivi sasa wanakaribisha wafadhili wenye mapenzi watakaotaka kuisaidia timu hiyo na kwamba wanachama wako tayari kukubali timu iitwe jina lolote ikiwa chini yao ili mradi iendelee kufanya vizuri katika medani ya mchezo wa mpira wa miguu hapa nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post